Featured Kitaifa

RAIS SAMIA ATOA MIL 361.1 KWA AJILI YA VIKUNDI VYA WANAWAKE VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU WILAYA YA USHETU//MBUNGE CHEREHANI AKABIDHI HUNDI WANUFAIKA

Written by mzalendoeditor

Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan imetoa mkopo wa Shilingi milioni mia tatu sitini na moja na laki moja (361,100,000) kwa ajili ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga.

Akizungumza wakati akikabidhi hundi katika hafla iliyofanyika Wilayani Ushetu tarehe 4 Februari 2023, Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe Dkt Emmanuel Peter Cherehani amesema kuwa fedha hizo ni maelekezo ya serikali kwa Halmashauri zote nchini kutoa Asilimia 10 ya mapato kwa ajili ya makundi hayo muhimu.

Dkt Cherehani amewataka wanufaika hao wa mkopo kuhakikisha kuwa wanatumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kujikwamua na wimbi la umasikini na si vinginevyo.

Amewasihi wanufaika hao kutumia vizuri mikopo hiyo na kuhakikisha kuwa miradi waliyokusudia kutekeleza wanaifanyia kazi ipasavyo ili waweze kurejesha mikopo kwa ajili ya kukopeshwa watu wengine.

“Pelekeni fedha kwenye eneo lililokusudiwa, ninajua wakati mwingine mnapata ushawishi kutoka kwa watu wengine lakini fedha hizi sio za kwenda kuhonga, kafanyeni maendeleo yenu na familia zenu” Amekaririwa Dkt Chereheni

Amesema kuwa fedha hizo hazipaswi kuwa sehemu ya mtafaruku katika familia badala yake ziwe sehemu ya kuimarisha umoja na mshikamano ndani ya familia.

Pamoja na kukabidhi fedha hizo kwa wanufaika hao pia Mhe Cherehani amekabidhi pikipiki kwa vijana kwa ajili ya kufanya biashara ya Bodaboda itakayowaingizia kipato.

Amewasihi wanufaika hao kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa bidii ili kuweza kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.

Mikopo hiyo imetolewa kwa vikundi 17 kati ya vikundi 70 vilivyoomba mikopo ambapo vikundi 11 ni vya wanawake, vikundi vitano ni vya vijana huku kikundi kimoja kikiwa cha watu wenye ulemavu.

Nao wanufaika wa mikopo hiyo ambao ni wakazi wa Ushetu wamempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mikopo hiyo kupitia Halmashauri za Wilaya huku wakisema kuwa watafanya kazi kwa bidii ili kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.

About the author

mzalendoeditor