Featured Kitaifa

SERIKALI YAANZISHA MIFUMO YA KUMUWEZESHA MWANANCHI KUFAHAMU HUDUMA ZINAZOTOLEWA NA TAASISI YA UMMA

Written by mzalendoeditor

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma kuelezea utekelezaji wa Mkataba wa Huduma kwa Mteja katika Taasisi za Umma nchini.

Waandishi wa Habari wakiwa katika kwenye mkutano na wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na Vyombo vya Habari jijini Dodoma alipokuwa akielezea utekelezaji wa Mkataba wa Huduma kwa Mteja katika Taasisi za Umma nchini.

…………………………………

Na Alex Sonna-DODOMA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya tumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama,amesema kuwa Ofisi yake imeanzisha utaratibu wa kutumia mifumo ambao inamuwezesha mwananchi kufahamu huduma zinazotolewa na Taasisi ya Umma.

Hayo ameyasema leo Januari 31,2023 jijini Dodoma wakati  akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa mkataba wa huduma kwa mteja katika utumishi wa umma.
Waziri Mhagama amesema kuwa Mifumo hiyo itamwezesha mwananchi kujua viwango vya utoaji wa huduma, wajibu wa taasisi kwa mpokea huduma, wajibu na haki ya mteja au mpokea huduma, njia zitakazomuwezesha mteja kupokea na kutoa mrejesho wa huduma  zilizotolewa na njia za mawasiliano na taasisi.
“Serikali ilishatoa Mwongozo wa kuziwezesha taasisi za umma kuandaa, kuhuisha na kutekeleza mkataba wa huduma kwa mteja. Utekelezaji wa mkataba huo ni dhamira ya serikali ya awamu ya sita  ya kuimarisha utamaduni wa watumishi wa umma nchini na utoaji wa huduma bora kwa wananchi kwa hiari na bila shuruti na  kuimarisha nidhamu na uwajibikaji,”almesema
Hata hivyo Waziri Mhagama, amesema Ofisi hiyo imebaini uwepo wa  baadhi ya Taasisi za Umma ambazo hazina Mkataba wa Huduma kwa Mteja, na zingine mikataba yao imeshapitwa na wakati au kuandaliwa bila kuzingatia Mwongozo wa Serikali wa kuandaa Mikataba.
 Amesema kuwa Taasisi hizo kwa kutozingatia Mwongozo wa uandaaji wa Mikataba ya Huduma kwa Mteja imepelekea Taasisi kuwa na Mikataba isiyokidhi viwango vya huduma vinavyotakiwa kutolewa, na hii ni kutokana na kukosekana kwa utayari wa Viongozi wa Taasisi za Umma kubadilisha mitizamo ya kiutendaji, kukubali mabadiliko na kuendelea kufanya kazi kwa mazoea kwenye Taasisi zao.
“Ofisi imebaini baadhi ya Taasisi za Umma hazifanyi ufuatiliaji wa utekelezaji wa mkataba na kuandaa taarifa na kuiwasilisha kwenye Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora hali inayosababisha Taasisi hizo kuendelea kufanya kazi kwa mazoea bila matokeo tarajiwa,”
Na kuongeza kuwa “Ofisi pia imebaini baadhi ya Taasisi kuandaa/kuhuisha mikataba ya Huduma kwa Mteja bila kushirikisha Wataalam husika na kupata idhini ya matumizi kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,”amesema Mhagama

About the author

mzalendoeditor