Featured Kitaifa

WAZIRI BASHUNGWA AFUNGUA MKUTANO MKUU WA MAJESHI NA MAKAMANDA WA JWTZ 

Written by mzalendoeditor

 

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Innocent Bashungwa amefungua mkutano wa sita wa Mkuu wa Majeshi na makamanda wa jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania uliofanyika Mjini Songea Mkoani Ruvuma huku akisisitiza wakuu wa vikosi kulinda maeneo yao yasivamiwe na wananchi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo Mhe. Bashungwa amewataka Wakuu wa Vikosi, shule na vyuo kuhakikisha wanalinda maeneo waliyopewa ili kuepuka migogoro ambayo hutokea mara kwa mara.

“Wakuu wa vikosi, shule na vyuo muhakikishe mnalinda maeneo yenu mliyopewa kuyasimamia na kuhakikisha mnayapima na kupata hati milki za maeneo hayo ili tuepuke migogoro inayotokea baada ya maeneo kuvamiwa” amesema Mhe. Bashungwa.

Katika hatua nyingine amesema jeshi la ulinzi limeendelea kuwa na mahusiano mazuri na majeshi mengine sambamba na vyombo vya ulinzi na usalama nchini.

“mahusiano na majeshi ya nchi jirani katika  mazoezi ya pamoja ya kikanda na majukumu ya kulinda amani  ni mazuri nidhamu, utii, uhodari, ujasiri na uaminifu kwa maafisa na askari ni wa hali ya juu na huu ni mchango wa usimamizi wa maafisa na Mkuu wa Majeshi” amesema.

Pia amempongeza Rais wa awamu ya sita Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassa kwa kuendelea kuliwezesha jeshi na kubainisha kuwa  serikali itaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuriboresha jeshi kwa raslimali watu, zana na vifaa.

Kwa upande wake Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Jacob Mkunda amezishukuru Serikali za awamu zote kuliwezesha jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania kutekeleza majukumu yao.

Katika hatua nyingine Jenerali Mkunda ameahidi kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria na kuhakikisha jeshi lipo timamu na tayari kukabidhiwa majukumu litakayopangiwa na serikali.

Ameongeza kuwa “Tumekutana hapa ili kujenga uelewa wa pamoja na kuweka mikakati ya ulinzi wanchi pamoja na kushirikishana changamoto mbalimbali na miongozo ya kazi” amesema Jenerali Mkunda.

About the author

mzalendoeditor