Waamini wa Parokia Teule ya Mt.Cecilia-Muungano Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma,wakiwa katika Ibada ya Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara kwa Wakristo 60,katika Parokia hiyo Teule ya Mt.Cecilia-Muungano.
Vijana waliomarishwa kwa mapaji saba ya Roho Mtakatifu wakiwa katika Adhimisho la Sadaka ya Misa Takatifu ya utolewaji wa Sakramenti ya Kipaimara, katika Parokia Teule ya Mt.Cecilia-Muungano Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma. (Picha na zote na Ndahani Lugunya)
………………………………………
Na Ndahani Lugunya,Dodoma.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Mhashamu Beatus Kinyaiya,ametoa wito kwa wazazi na walezi hasa akina Mama kuacha kutoa adhabu zinazozidi kiwango kwa watoto kiasi cha kupelekea madhara kwao kimwili na kisaikolojia.
Ametoa wito huo wakati akitoa homilia yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara kwa Wakristo 60,katika Parokia Teule ya Mt.Cecilia-Muungano Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.
Askofu Mkuu Kinyaiya amesema wapo baadhi ya akina Mama wanapokorofishana na wenza wao, wamekuwa wakitoa adhabu zisizostahili kwa watoto kutokana na hasira wanazokuwa nazo jambo ambalo limekuwa likipeleka madhara makubwa kwa watoto na hata kupoteza maisha.
“Kwa namna ya pekee naomba akina Mama msitumie hasira zenu kuumiza watoto.mmekorofishana na bwana wako unakwenda kumalizia hasira kwa mtoto.nalisema hilo kwa sababu matukio ya namna hiyo yamekuwa yakitokea tena na tena .
Kuna akina Mama wanapiga watoto mpaka wanawaharibu.wengine wanachukua wembe wana wachanachana.ukimuuliza anakwambia nilikuwa na hasira kwa sababu ya baba yake.sasa mama mtoto amekukosea nini,labda amekosea kidogo tu adhabu unayompa haiendani na kosa si sawa hiyo,” amesema Askofu Kinyaiya.
Pamoja na suala la adhabu za kupitiliza,amewataka pia akina mama kuacha kuchukua maamuzi yenye kuleta madhara kwa familia na hata jamii kwa ujumla kutokana na hasira,pale inapotokea hali ya kutokuelewana baina yao na wenza wao.
“Naomba akina Mama msipate hasira mkafanya mambo ambayo hayastahili.na linaloendana na hilo ni hasira,unapokuwa na hasira nakuomba usifanya maamuzi uwe Baba Mama Padri au Kiongozi usifanye maamuzi ukiwa na hasira.
Unapotaka kufanya jambo ukiwa na hasira nenda chumbani ukajifungie usali na utulie,ukishatulia rudi utaamua tofauti na ulivyotaka kufanya hapo awali,’amesema Askofu Kinyaiya.
Hata hivyo ametoa wito kwa familia za Kikristo kuona umuhimu wa kujitoa kwa moyo katika kutimiza wajibu msingi wa kiroho na kimwili kwa kila mwanafamilia.
Amesema kuwa malezi bora ni lazima yashirikishe familia yote ikiongozwa na Baba na Mama pasipo mmoja wapo kukwepa majukumu yake,ili watoto walelewe katika misingi bora mfano wake ukiwa ni familia ya Yesu,Maria na Yoseph.
“Kila familia ione umuhimu wa kujitoa kabisa,kama wewe ni mwanafamilia yaani Baba,Mama au mtoto la kwanza ni kujitoa kabisa katika kutimiza wajibu.Yoseph Maria na mtoto Yesu kinachowafanya wawe watakatifu ni kule kujitoa jumla katika majukumu yao ya kawaida ya kila siku.
Yoseph pamoja na kuwa Baba mlishi lakini alijua anawajibu ule ule kama Baba wa kuhakikisha mtoto anakua na kulelewa vizuri kama watoto wengine,vivyo hivyo na Yesu nae aliwajibika kwelikweli katika shughuli za uselemala alizokuwa akizifanya baba yake Yoseph nayeye alizifanya.
Kwa hiyo naomba kila mmoja akumbuke wajibu wake katika familia na autimize vizuri.watoto muwe watii kwa wazazi,muwe watii kwa walimu na mfanye kazi zinazo wahusu zikiwemo za shuleni na nyumbani,” amesema Askofu Kinyaiya.
Askofu Kinyaia amezitaka familia ziwe na mawasiliano ya mara kwa mara, ili kujadiliana mipango mbalimbali ikiwemo masuala ya kiimani na kuziimarisha Parokia yao.
Aidha amewataka waumini ambao hawajafunga ndoa kutekeleza wajibu wao wa kiimani na kujenga tabia ya kusameheana pale wanapokoseana kuanzia kwenye familia hadi Kanisani.
“Kama watoto wa kiroho naomba tutekeleze majukumu yetu ya kiroho tunayoelezwa na Viongozi wetu wa kiroho akiwemo Baba Paroko pamoja na Viongozi wetu katika ngazi ya Jumuiya hadi Parokia,” amesema Askofu Kinyaiya.
Hata hivyo Askofu Kinyaiya amehitimisha homilia yake kwa kuwaalika waamini na watu wote kila mmoja kwa nafasi yake, katika mwaka huu wa 2023 kujitahidi kupanda ngazi ya mabadiliko kiroho na kimwili.
Pamoja na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara, Askofu Mkuu Kinyaiya amebariki nyumba ya Mapadri pamoja na tarbernakulo kwa ajili ya kuhifadhi hostia takatifu Parokiani hapo.
Ikumbukwe kwamba Parokia teuele ya Mt.Cecilia-Muungano ambayo ipo chini ya Parokia ya Mt.Gemma Galgan-Nkuhungu,ni miongoni mwa Parokia 51 za Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma,ambapo itazinduliwa rasmi kuwa Parokia kamili Oktoba 15 mwaka huu.