NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Mauld Mwita, ameahidi kuvalia njuga changamoto zinazowakabili waandishi wa habari wa vyombo vya binafsi ili wanufaike na kazi wanazozifanya kwenye vyombo hivyo.
Ameeleza jhayo Disemba 26, 2022 wakati akifungua mkutano mkuu maalum wa Klabu ya waandishi wa habari Zanzibar (ZPC), uliofanyika katika ukumbi wa Uhuru uliopo katika viwanja vya kufurahishia watoto Kariakoo Zanzibar.
Ameeleza kuwa anatambua changamoto zinazowakabili waandishi na watendaji wa vyombo vya habari hasa vya binafsi hivyo atafanya ziara za kushitukiza ili kujionea na kuona hatua za kuchukua kustawisha hali za wafanyakazi wa vyombo hivyo.
Swala la wafanyakazi wa vyombo binafsi kutokua na mikataba nalifahamu lakini pia nafahamu mambo mengi ndio maana nmepanga kufanya ziara za kushitukiza ili nikajionee mwenyewe na nitachukua hatua kwa kushirikiana na taasisi au wizara nyengine,” amesema Tabia.
Aidha waziri huyo amepongeza kazi kubwa zinazofanywa na vyombo vya habari na kuvitaka kuendelea kufanya hivyo kwa kuzingatia misingi ya taaluma, sheria na maadili huku akiahidi kwamba serikali itaendelea kuweka mazingira ya kisera na kisheria kwa lengo la kuiimarisha kada ya uandishi wa habari.
Akizungumzia mchakato wa upatikanaji wa sheria mpya ya habari, Waziri huyo ameeleza kuwa unaendelea vyema na kwamba mswada wa sherisa hiyo unatariwa kupelekwa katika baraza la wawakilishi katika vikao vya awali ya mwaka ujao wa 2023.
Akimkaribisha Waziri Tabia, Mwenyekiti wa ZPC, Abdallah Mfaume, alimuomba kusimamia na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wandishi wa habari wa vyombo vya habari binafsi ili wafanye kazi kwa ufanisi zaidi.
Mfaume amesema waandishi hao wanakabiliwa na changamoto za kutolipwa stahiki zao kwa wakati kunakosababishwa na baadhi yao kutokuwa na mikataba ya ajira jambo linalodhoofisha utendaji wao.
Aidha amezungumzia haja ya kurejeshwa kwa posho la mazingira magumu walilokua wakilipwa waandishi wa habari wanaofanya kazi katika vyombo vya serikali kwani kazi wanazofanya zinalingana na watumishi wengine wanaolipwa posho hilo.
Awali akitoa maelezo ya mkutano huo, Katibu Mkuu wa ZPC, Mwinyimvua Nzukwi, ameeleza mkutano huo ni maalum kwa ajili ya kupitia na kuridhia mipango na maazimio ya mabadiliko ya kiutendaji naliyoanza kutekelezwa na Muungano wa Klabu za Waaandishi wa habari Tanzania (UTPC).
Ameeleza kuwa katika utekelezaji wa majukumu yake, zpc na utpc imeamua kuchukua hatua za kuimarisha utendaji chini ya kauli mbiy ya ‘kutoka ubora kwenda ukubwa’ inayolenga kuziimarisha taasisi hizo.
Katika mkutano huo pamoja na kuchangia taarifa zilizowasilishwa walipendekeza na kuthibitisha majina ya wajumbe wa bodi, wajumbe wa kamati ndogo ndogo, kufanya mabadiliko ya katiba na kuridhia kwa kauli moja maazimio yaliyofikiwa katika mkutano mkuu maalum wa utpc uliofanyika jijini Dar es salam Disemba 7, 2022.