Featured Kitaifa

KAYA 156,586 ZAUAGA UMASIKINI KUPITIA TASAF 

Written by mzalendoeditor

MKURUGENZI Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Ladislaus Mwamanga,akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 20,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu uhitimu wa walengwa walioimarika kiuchumi kupitia uwezeshwaji uliofanywa na mfuko huo.

………………………………….

Na Alex Sonna-DODOMA

JUMLA ya Kaya  156,586 zimeondolewa katika Mfuko wa Maendeleo ya Jamii ( TASAF) baada ya kuimarika kiuchumi ambapo sasa zinaweza kujitegemea pasipo kupata ruzuku.

Kaya hizo ni miongoni mwa kaya zaidi ya Milioni 1.3 zilizo katika kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya mpango huo kilichozinduliwa Februari 2022,ambapo kuondolewa kwake ni baada ya kufanyika tathimini ya hali za ustawi wa maisha yao katika mamlaka zote 186 za utekelezaji.

Hayo yalielezwa leo Desemba 20,2022 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Ladislaus Mwamanga,wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu uhitimu wa walengwa walioimarika kiuchumi kupitia uwezeshwaji uliofanywa na mfuko huo.

Mwamanga amesema kuwa  kwa sasa kaya hizo zina makazi bora, zinaweza kumudu gharama za matibabu, kusomesha watoto na zina vitega uchumi na biashara za uhakika zinazoongeza pato la familia.

“Kwa mujibu wa taratibu za muundo wa mpango, kaya inaponufaika hatua ya kujikimu na kuimarika kiuchumi kwa kuwa na chanzo au vyanzo vya uhakika wa mapato, inapoteza sifa za kuendelea kupokea ruzuku na inadi iondolewe kwenye mpango,” amesema Bw.Mwamanga

Hata hivyo Mwamanga amesema pamoja na kaya hizo zipo kaya nyingine 16,490 ambazo pia zitatolewa kwenye mpango ifikapo Januari mwaka 2023.

Amesema kuwa Kaya hizo zimetoka katika halmashauri za wilaya ya Bagamoyo,Kibaha,Lindi,Chalinze na katika manispaa za Mtwara,Lindi na kutoka Unguja.
Mwamanga amesema kuwa  TASAF itaendelea kutoa elimu kwa walengwa kuhusu taratibu za Mpango kuhamasisha ushiriki wa walengwa katika masuala mbalimbali kuwekeza ili wanapohitimu waweze kujihudumia wao wenyewe.

Aidha ametaja njia zilizotumika kuwatambua na kuwaondoa kwenye mpango kuwa ni kuitisha mikutano ya kijamii,kujaza dodoso la taarifa za hali ya uchumi ya kaya na kufanya uhakiki kwa kutumia mfumo maalum wa kuchakata takwimu kwa njia ya kompyuta.

Mpango wa kunusuru kaya maskini ulianza 2012 ambapo mpaka kipindi cha kwanza kinakamilika Disemba 2019 kulikuwa na walengwa zaidi ya Milioni 1.1 kutoka asilimia 70  ya vijiji,Mtaa,shehia zote nchini pamoja na Zanzibar.

About the author

mzalendoeditor