Featured Kitaifa

ORYX,KAMPUNI ZA MAFUTA KUIMARISHA MIUNDOMBINU YA USALAMA

Written by mzalendoeditor
Mkurugenzi wa Oryx Energies ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Waagizaji na Wasambazaji wa Mafuta Tanzania (TOAMAC)Kalpesh Mehta akizungumza na wadau mbalimbali wanaohusika na masuala ya kukabiliana na majanga pamoja na wakurugenzi wa kampuni mbalimbali za mafuta zilizopo Kurasini Dar es Salaam jana baada ya kufanyika kwa zoezi la kukabiliana na majanga ambalo limefanyika kwenye kampuni ya Oryx.Ametumia nafasi hiyo kueleza kwamba wadau hao wataendelea kushirikiana katika kuendelea kufanya mazoezi ya kukabiliana na majanga ili kuwa na utayari.(Na Mpiga picha Wetu) 
………………………
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KAMPUNI Oryx Energies kwa kushirikiana na kampuni nyingine za uagizaji na usambazaji mafuta nchini, wameshirikiana kuendesha zoezi la kukabiliana dhidi ya majanga katika maeneo ya shughuli zao huku zikiahidi kuendelea kuimarisha miundombinu ya usalama katika maeneo yao ya kazi.
Zoezi hilo la kukabiliana dhidi ya janga la moto limefanyika katika Kampuni ya Oryx Energies Kurasini jijini Dar es Salaam, jana ambapo limeshuhudiwa na wakurugenzi na maofisa wa kampuni za mafuta chini ya mwavuli wa Chama cha Waagizaji na Wasambazaji Mafuta Tanzania (TOAMAC), Jeshi la Polisi, Jeshi la Zima Moto, wawakilishi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na madereva.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa zoezi hilo, Mkurugenzi wa Oryx Energies ambaye pia ni Mwenyekiti wa TOAMAC, Kalpesh Mehta, alisema ni jambo la msingi kwa kampuni za mafuta kuhakikisha zinakuwa na utayari wa kukabiliana na majanga katika maeneo ya shughuli zao.
“Majanga yanayoweza kutokea kwenye kampuni zetu, muhimu kuona kunakuwa na usalama wa kila mtu. Watu wanaoishi maeneo yaliyokaribu na matanki ya kuhifadhia mafuta na maeneo mengine lazima wawe na utayari wa kuabiliana na majanga yanapotokea, hivyo nasi kwa nafasi yetu tumeamua kufanya zoezi la kujiandaa ili kujilinda na kulinda majirani zetu,” alisema Mehta.
Alisema wanatambua eneo la Kurasini ndiko ilikokuwa Bandari ya Dar es Salaam ambao ni mlango wa uchumi unaohudumia nchi sita zinazoizunguka Tanzania, hivyo lazima wahakikishe kuna usalama wa kutosha.
Kuhusu ombi la Kamanda wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Temeke, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto, Maria Luwoga, la kuzitaka kampuni za mafuta eneo la Kurasini kuangalia namna ya kushirikiana kununua mtambo wa kuzimamoto utakaokuwa eneo hilo lenye matanki ya mafuta, amesema ni wazo zuri na watakaa kupitia Chama chao waone wanaweza kufanya nini kwenye hilo.
Alisema amefurahishwa na wadau ambao wameshiriki kikamilifu huku akiahidi zoezi lingine litakalokuja yale mapungufu ambayo yameonekana tayafanyiwa kazi.
Kwa upande wake Meneja Operesheni wa Kampuni ya Oil Com, Salehe Islam, alisema wanavipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kutoa ushirikiano wa kuhakikisha sheria za kukabiliana na majanga nchini zinafuatwa. 

About the author

mzalendoeditor