Featured Kitaifa

ASKOFU KINYAIYA ASISITIZA UTUNZAJI NA UHIFADHI WA MAZINGIRA.

Written by mzalendoeditor

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Mhashamu Beatus Michael Kinyaiya OFM Cap,akitoa homilia wakati wa Ibada ya Misa Takatifu ya utoaji wa Sakramenti ya Kipaimara katika Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa ledochowska-Kiwanja cha Ndege Dodoma Makulu.(Picha na Ndahani Lugunya)

…………………….

Na Ndahani Lugunya,Dodoma.

Askofu Mkuu wa Jimbo kuu katoliki la Dodoma Beatus Micheal Kinyaiya, amekazia waraka wa Baba Mtakatifu fransisco wa Laudato Si kuhusu utunzaji wa mazingira kwa kuwataka waamini wote na watu wote wenye mapenzi mema kutunza mazingira nyumba yetu ya pamoja.

Amesema hayo wakati akitoa homilia yake kwenye Adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu ya utoaji wa Sakramenti ya Kipaimara kwa Vijana 180, katika Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowsca Kiwanja cha ndege Jimboni Dodoma.

Katika homilia yake Askofu Kinyaiya amewaomba na kuwahimiza waamini na watu wote kila mmoja kutambua wajibu msingi wa kutunza,kujali na kuhifadhi mazingira,kama sehemu ya kuheshimu kazi ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu.

“Tutunze dunia hii ambayo ni mama yetu.Mungu aliiumba akatukabidhi sisi wanadamu tuitunze lakini kwa sababu ya uvivu wetu tunaiharibu dunia.tunashindwa kuijali kwa sababu ya uzembe wetu.mtu anakunywa maji chupa anaitupa popote pale anapojisikia.dunia imekuwa sio nzuri kama ilivyokuwa kwa sababu ya mwanadamu kutoijali,” amesema Askofu Kinyaiya.

Sanjari na hayo Askofu Kinyaiya amesisitiza suala la amani katika familia,jamii na Taifa kwa ujumla kama ambavyo Kristo Yesu alitaka amani itawale kwa kila mtu  ulimwenguni kote.

“Aliyofundisha Yesu katika ujio wake pamoja na mambo mengine ilikuwa ni kutuhamasisha sisi tuwe watu wa amani.kwa hiyo kama Jumuiyani hakuna amani kuna migogoro na vita ya maneno ni chanzo cha matatizo katika jamii,” amesema Askofu Kinyaiya.

Amesema matatizo ya migogoro na migongamano mingine katika jamii inasababishwa na ulafi wa mali pamoja  na uvivu kwa badhi ya watu kutotoka kujishughulisha ili kujipatia mali za halali,jambo linalopelekea kukosekana kwa amani ndani ya jamii.

Hata hivyo Askofu Kinyaiya amewataka waimarisha wa mapaji saba ya Roho Mtakatifu kutambua baada ya kupata Sakramenti ya Kipaimara wanakuwa watu wazima kiimani.

Amesema licha ya umri wa vijana hao kuwa ni wadogo lakini Kanisa linaamini wanaelewa mambo ya msingi yawapasayo kufanya  kutokana na mafundisho ya msingi ambayo wamepewa kutoka katika Katekisimu na Biblia yanayo wasaidia kusimama kiimani.

“Wewe mwenyewe uishi yale Mungu anayokuamuru uishi yaani maadili na mafundisho ya Kanisa lakini pia uwasaidie wengine kuelewa na kuishi lakini utawasaidia  endapo wewe mwenyewe unaelewa,” amesema Askofu Kinyaiya.

Amesema moja ya changamoto ambayo watakutana nayo ni kwa baadhi ya makanisa yanayoibukia kuhoji Kanisa Katoliki kutumia vitu vingine kufundisha mafundisho yake ikiwemo mapokeo,badala ya kutumia Maandiko matakatifu pekee,kumbe wao kama Askari hodari wa Kristo na Kanisa lake wawafundishe wale wote wanaohoji juu ya mafundisho ya Kanisa.  

About the author

mzalendoeditor