Featured Kitaifa

ALHAJ OTHMAN AENDELEA KUSISITIZA WAJIBU WA KUTENDA HAKI NA UADILIFU

Written by mzalendoeditor

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Alhaj Othman Masoud Othman, leo Disemba 02, 2022 amejumuika na Waumini mbali mbali wa Kiislamu, katika Ibada ya Sala ya Ijumaa, hapo Masjid Tukadim, Msikiti wa Asili wa Shumba Mjini, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini, Pemba.

Katika salamu zake kwa Waumini, Mheshimiwa Othman aliyepo ziarani kisiwani Pemba, amehimiza uadilifu kwa jamii, akisema kuwa sasa jamii imekumbwa na janga la ubadhirifu, ambapo msingi mkubwa wa kukabiliana nalo unaasisiwa tangu malezi ya watoto.

Ibada hiyo iliyowajumuisha Viongozi mbali mbali wa Serikali, Dini, Siasa na Jamii, imehusisha pia Dua Maalum ya Kumuombea Mh. Othman.

Dua hiyo imeongozwa na Imamu Mkuu wa Msikiti huo, Sheikh Omar Khamis Makame, ambaye ametaja kuwa ni ikram maalum kwa Kiongozi huyo ambaye wamemchukulia kama faraja na furaha kubwa kijijini hapo.

Kabla ya Dua hiyo, Khatib Sheikh Haji Masoud Kombo, ametoa Khutba Mbili za Ijumaa zilizoweka msisitizo kwa Waumini, juu ya umuhimu wa kutekeleza imani ya Dini kwa vitendo, ikiwemo uadilifu kama ilivyosisitizwa katika Misingi ya Dini ya Kiislamu.

Mapema kabla ya ibada ya Sala ya Ijumaa, Mheshimiwa Othman, alipata fursa ya kubadilishana mawazo na Wazee wa kijiji hicho cha Shumba Mjini pamoja na kusalimiana na Wananchi.

Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar

About the author

mzalendoeditor