Featured Kitaifa

WAZIRI NDALICHAKO:’NCHI ZA SADC KUWEZESHA KULINDWA HAKI ZA WAHAMAJI KAZI’

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof, Joyce Ndalichako amesema nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimeazimia kutekeleza Sera, Mikakati na programu zitakazowezesha kulindwa kwa haki za msingi za wahamaji wa kazi katika nchi hizo.  

Waziri Ndalichako ameyabainisha hayo mara baada ya kushiriki Mkutano wa Utatu wa Mawaziri wa Kazi na Ajira na Wadau wa Utatu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), uliofanyika kuanzia tarehe 29 – 30, nchini Zimbabwe.

Amefafanua Mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuwekeza kwenye ukuzaji ujuzi, kuimarisha mifumo ya utoaji wa vibali vya kazi na ukaazi, hifadhi ya jamii kwa wahamaji wa kazi.

Aidha, Mhe.Prof.Ndalichako amesisitiza kuwa Mkutano huo umeazimia kuhakikisha shughuli za mawakala binafsi wa ajira zinazingatia viwango vya kazi za staha.

Katika hatua nyingine, katika mkutano huo Tanzania imetoa uzoefu wake namna inavyoratibu masuala ya uhamaji wa nguvukazi ikiwemo, kuweka mifumo rafiki ya kielektroniki ya utoaji wa vibali vya kazi na ukaaji kwa raia wa kigeni.

Masuala mengine ambayo Tanzania imeyatolea uzoefu ni pamoja na kuanzisha pasi maalum kwa wafanyakazi wa musimu pamoja na utekelezaji wa programu ya mafunzo ya ukuzaji ujuzi kwa vijana kuwa na ujuzi wa kuajirika ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika, Bibi. Cynthia Samuel Olonjuwon ameshauri nchi za SADC kushirikiana katika kuandaa na kutekeleza sera zitakazowezesha uhamaji wa nguvukazi ndani na nje ya SADC unafanyika kwa kuzingatia viwango vya kazi za staha.

Naye, Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya katika Jumuiya ya SADC, Balozi Petra Pereyra ameeleza kuwa EU iko tayari kuziwezesha nchi za SADC kuwa na sera imara za uhamaji wa nguvukazi.

Awali akifungua Mkutano huo Rais wa Zimbabwe Mhe. Dr. Emmerson Mnangagwa ambaye aliwakilishwa na Makamu wa Rais wa Zimbabwe Mhe. Jenerali Dkt. Constantino Chiwenga alizishauri nchi wanachama wa SADC kutazama uhamaji wa nguvukazi katika nyanja ya kimaendeleo inayohitaji uratibu wa pamoja.

Mkutano huo uliojikita kwenye nguvukazi ulihudhuriwa na Mawaziri 9, Manaibu Mawaziri 3, Makatibu Wakuu; Wataalam kutoka nchi wanachama wa SADC; Wawakilishi wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri pamoja na Wawakilishi wa Taasisi/Jumuiya za Kimataifa.

Kwa upande wa Tanzania katika mkutano huo Mhe. Prof. Ndalichako ameambatana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Isaac Maduhu,Naibu Katibu Mkuu – TUCTA; Kanali Lucas Magembe, kutoka ATE Bibi. Mercy Patric; kutoka Chama cha Wafanyakazi Zanzibar, Mwanamkuu Gharib Mgeni na Ofisi ya Waziri Mkuu, Joseph Nganga pamoja na Eliud Ikomba kutoka Idara ya Uhamiaji.

About the author

mzalendoeditor