Featured Kitaifa

CCM:SHAHADA YA UDAKTARI KWA RAIS SAMIA NI MATOKEO YA KAZI KUBWA,NZURI

Written by mzalendoeditor

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitunukiwa Shahada ya Udaktari wa Falsafa wa Heshima ikiwa ni Shahada ya Udaktari wa Juu katika Humanitia na Sayansi Jamii na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Rais Mstaafu wa Awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete katika Mahafali ya Hamsini na mbili (52) ya Duru ya Tano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City tarehe 30, Novemba, 2022. 

……………………..

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kutunukiwa Shahada ya udaktari wa Falsafa ikisema hatua hiyo inadhihirisha na kusadifu kazi kubwa na anayoitekeleza kiongozi huyo mkuu wa nchi.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Chama jana na kutiwa saini na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka ikisema kazi kubwa na nzuri inayofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia ni chachu ya kutolewa kwa Shahada hiyo.

“Tumeguswa na kufurahishwa na uamuzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kumtunuku shahada ya udaktari wa heshima Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan katika mahafali ya 52 duru ya 5 yaliyofanyika Novemba 30, 2022 (jana) katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

“Uamuzi huo ni uthibitisho wa dhahiri wa kazi kubwa na nzuri inayofanywa na serikali ya CCM ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuleta ustawi wa maisha na maendeleo endelevu kwa nchi yetu,” alisema.

Shaka alisema kati ya kazi kubwa iliyofanyika na kutumika kumtunuku shahada hiyo ni pamoja na mageuzi ya kiuchumi, kuimarisha misingi ya demokrasia, utawala bora na kuleta maendeleo ya jamii.

“Ameleta furaha na tumaini jipya miongoni mwa wananchi. Yote hayo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 uliochagizwa na utashi wake wa kisiasa, ukomavu na umahiri alionao katika uongozi,” alisema.

Shaka alisema shahada hiyo ni fahari kwa Chama na Watanzania wote ikionyesha kuwa nchi ina Rais anayewajibika kwa maslahi ya wote na kwamba itampa moyo kuwa wananchi wanaona kazi nzuri anazozifanya kwa taifa hivyo kumpa ari na nguvu ya kuendelea kutekeleza wajibu wake.

Shahada hiyo alitunukiwa jana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika mahafali ya 52 duru ya 5 yaliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam

About the author

mzalendoeditor