Featured Kitaifa

WAZIRI MKENDA ATETA NA VIONGOZI WA TAHLISO,ZAHLIFE JIJINI DODOMA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ameahidi kushughulikia changamoto mbalimbali za wanafunzi wa elimu ya juu zilizowasilishwa na viongozi wa Jumuiya ya wanafunzi wa Taasisi ya Elimu ya Juu ikiwemo uimarishaji wa uhusiano kati ya Jumuiya hiyo, Tume ya Vyuo Vikuu, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na NACTVET.

Waziri Mkenda amesema hayo Jijini Dodoma leo Novemba 28, 2022 wakati wa kikao cha pamoja na Jumuiya hiyo ambapo amesema wanafunzi ni wadau wakubwa kwenye elimu hivyo ni vizuri kushughulikia changamoto zao ili wasome katika mazingira mazuri.

Waziri Mkenda amewaeleza viongozi hao yapo mambo mengi ambayo Serikali imefanya katika kuhakikisha wanafunzi wa elimu ya juu wanasoma katika mazingira mazuri ikiwemo kuongeza fedha ya mikopo kwa wanafunzi kutoka Sh. bilioni 570 hadi kufikia bilioni 654.

“Wakati Rais Samia anaingia madarakani mikopo ya wanafunzi ilikuwa Sh. bilioni 464 akaongeza na kufika bilioni Sh. bilioni 570 lakini hata sasa ameongeza na Sh bilioni 84 na kufika Sh bilioni 654 lengo ni kuhakisha wanaostahili kupata mikopo wanapata”

Amesema pamoja na kuongeza fedha hizo Wizara kwa kushirikiana na Bodi inaendelea kuhakikisha mikopo inayotolewa inazingatia vigezo viliyowekwa vya utoaji mikopo.

Vilevile amesema katika kuongeza fursa za upatikanaji wa Elimu ya Juu Serikali imeanzisha ufadhili wa masomo unaojulikana kama Samia scholarship ambayo inatolewa kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita na kufaulu vizuri katika masomo ya sayansi na kuchagua kuendelea na masomo hayo Chuo Kikuu katika fani ya elimutiba, Sayansi na uhandisi.

“Hivi karibuni tutatangaza rasmi orodha ya wanufaika wa Samia Scholarship,” amesema Waziri Mkenda.

Kwa upande wake rais wa Serikali ya wanafunzi (TAHLISO) Frank Nkinda amemshukuru Waziri Mkenda kwa kukubali kukutana na viongozi wa jumuiya ya wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu na kwamba anaamini kupitia kikao hicho changamoto za wanafunzi wa elimu ya juu zinakwenda kutatuliwa.

Ameshukuru Rais kwa namna anavyoiwezesha Wizara kutekeleza majukumu yake ipasavyo na amemwomba Waziri Mkenda pamoja na kushughulikia suala la uwakilishi pia kumekuwa na changamoto ya mawasiliano na uhusiano baina ya maafisa mikopo na Bodi hivyo kuleta shida katika kutatua changamoto za wanafunzi wenye shida ya mikopo vyuoni.

Nae Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar (ZAHILFE) Mahmoud Maktuba ameishukuru Wizara kwa kuona umuhimu wa kukutana na viongozi wa jumuiya ya wanafunzi wa elimu ya juu Tanzania Bara na Visiwani ambapo amesema kwa kufanya hivyo ni kudumisha muungano ambayo ndio ndoto ya Watanzania wote na utatuzi wa changamoto za wanafunzi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa TAHLISO wamemshukuru Rais Samia kwa kuongeza mikopo ya wanafunzi wa elimu ya Juu, kufuta asilimia sita ya kutunza thamani ya fedha (rentetion fee). Pia wamempongeza Waziri Mkenda kwa namna anavyoonesha ushirikiano katika kushughulikia changamoto mbalimbali za wanafunzi wa elimu ya juu.

Kipekee Viongozi wa Jumuiya ya wanafunzi wa Taasisi za elimu ya Juu ( TAHLISO) wameipongeza Idara ya Elimu ya Juu ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa utoaji huduma na ushirikiano muda wakati wote.

About the author

mzalendoeditor