Featured Kitaifa

WAJUMBE WA BODI YA eGA WATAKIWA KUSIMAMIA VEMA UTENDAJI KAZI WA SERIKALI MTANDAO ILI KUEPUSHA VITENDO VYA RUSHWA 

Written by mzalendoeditor

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) jijini Dar es Salaam, mara baada ya ya Waziri huyo kuizindua bodi hiyo.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzindua Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Dkt. Musa Kissaka akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama, mara baada ya Waziri huyo kuzindua Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Mhandisi Benedict Ndomba akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya eGA kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka hiyo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akimkabidhi vitendea kazi Bw. Eric Shitindi ambaye ni mmoja wa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), mara baada ya Waziri huyo kuizindua bodi hiyo jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), mara baada ya Waziri huyo kuizindua bodi hiyo jijini Dar es Salaam. Wa pili kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI Bw. Xavier Daudi.

………………………………

Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewataka Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kusimamia vema utendaji kazi wa Serikali Mtandao ili kupunguza uwezekano wa wananchi kuathiriwa na vitendo vya rushwa.

Mhe. Jenista ametoa wito huo jijini Dar es Salaam, wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) ambayo imepewa jukumu la kuisimamia Mamlaka hiyo kuhakikisha inatekeleza wajibu wake. 

Mhe. Jenista amesema matumizi ya serikali mtandao yanawaepusha wananchi kukutana na watendaji hivyo kuondoa mazingira yanayoshawishi vitendo vya rushwa.

Amewataka Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya eGA kuweka mikakati madhubuti na imara itakayoiwezesha Serikali Mtandao kutatua changamoto zinazowakabili wananchi pindi wanapofuata huduma mbalimbali katika Taasisi za Umma.

“Ninasisitiza wajumbe wa bodi mjikite zaidi katika kuhakikisha mnaweka mikakati ya matumizi ya TEHAMA ambayo itaondoa changamoto ya upatikanaji wa huduma hasa kwa wananchi wa kawaida ambao Mhe. Rais amedhamiria kuwapatia huduma stahiki,”

Naye, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amesema kuwa, Wajumbe wa Bodi hiyo ya Wakurugenzi ya eGA wakitekeleza wajibu wao ipasavyo kwa kusimamia kikamilifu sera za serikali mtandao, wataisaidia Mamlaka ya Serikali Mtandao kulifikisha taifa katika uchumi wa kidijitali na mapinduzi ya nne ya viwanda, ikiwa ni pamoja na kuwezesha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Dkt. Musa Kissaka amesema wajumbe wa bodi anayoiongoza wamepokea majukumu na maelekezo ambayo Mhe. Jenista ameyatoa, na kuahidi kuwa watajitahidi kadiri ya uwezo wao kufanya kazi kwa bidii na weledi katika kuisimamia na kuiongoza Mamlaka ya Serikali Mtandao.

Akizungumzia utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya Serikali Mtandao, Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Mhandisi Benedict Ndomba amesema, mamlaka anayoiongoza imeendelea kusimamia na kuhimiza uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika Taasisi za Umma.

Mhandisi Ndomba ameongeza kuwa, Mamlaka ya Serikali Mtandao imeendelea kufanya kaguzi za mifumo ya TEHAMA, kufuatilia usalama wa Serikali Mtandao ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti na kutoa mafunzo ya Serikali Mtandao kwa watendaji wa Serikali.

About the author

mzalendoeditor