Featured Kitaifa

TANZANIA MWENYEJI MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA MKATABA WA UNESCO JUU YA URITHI WA ASILI NA KITAMADUNI.

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa kitengo cha sayansi asilia kutoka UNESCO Keven Robert, katikati ni Kamishna msaidizi mwandamizi wa uhifadhi kotoka mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro Mhandisi Joshua Mwankonda na kulia ni Joyce Mgaya mkuu wa kitengo cha mawasiliano kutoka NCAA wakiongea na waandishi wa habari katika semina hiyo iliyofanyika jijini Arusha.

mkuu wa kitengo cha sayansi asilia kutoka shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia masuala ya sayansi, elimu na utamaduni (UNESCO) Dar es salaam akiongea na wanahabari juu ya mkataba huo wa uridhi wa kidunia wa asili na kitamaduni.

Kamishna msaidizi mwandamizi wa uhifadhi kotoka mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro Mhandisi Joshua Mwankonda akiongea katika semina hiyo iliyofanyika mkoani Arusha.

……………………………..
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Tanzania kupitia mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imepewa jukumu la kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya miaka 50 ya mkataba UNESCO wa urithi wa kidunia wa asili na kitamaduni, mkataba ulioletwa mwaka 1972 na kuridhiwa na Tanzania mwaka 1977, maadhimisho yanayotarajiwa kufanyika Disemba 12 hadi 14, 2022.
Akiongea na waandishi wa habari katika semina ya kuelimisha wanahabari juu ya mkataba huo mkuu wa kitengo cha sayansi asilia kutoka shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia masuala ya sayansi, elimu na utamaduni  (UNESCO) ofisi ya Dar es salaam Keven Robert alisema kuwa maadhimisho hayo yatayoenda sambamba na mkutano unaolenga kuipa UNESCO, nchi wanachama pamoja na wadau kuweza kuangalia na kujadili mafanikio ya mkataba, changamoto zinazowakabili nchi wanachama pamoja na kijifunza utekelezaji wa mkataba huo kutoka kwa wadau mbalimbali.
“Tanzania imepewa jukumu la kuandaa mkutano huu kwasababu ni mwanachama wa UNESCO lakini pia ni miongoni mwa nchi za mwanzo kuridhiwa mkataba huu pamoja na kuwa na historia nzuri ya kutekeleza mkataba huu toka 1977 na kufanya  kuwa nchi ya mfano kwaajili ya kijifunza ikiwa ni pamoja na kuweza kutatua changamoto zinazo tokea katika maeneo haya kwa njia ya maridhiano,” Alisema Keven Robert.
Alisema pamoja na kuwa Tanzania ni mojawapo ya nchi wanachama zilizopo katika utekelezaji mzuri wenye mafanikio pia ina maeneo saba yaliyopo kwenye orodha ya urithi wa kidunia huku maeneo mengine saba yakiwa katika hatua ya kusubiri kuingizwa katika orodha hiyo.
“Maeneo yaliyotambulika na UNESCO kama urithi wa kidunia wa kitamaduni hapa Tanzania ni pamoja na Stone Town -Zanzibar, Kilwa kisiwani na Kondoa rock art, na ya asili ni Kilimanjaro, Serengeti na Selous pamoja na  eneo Ngorongoro ambalo ni la urithi mchanganyiko wa kimazingira na binadamu,” Alisema Keven Robert.
“Maeneo saba mengine hapa nchini yanayosubi kuingia kwenye orodha ya urithi wa kidunia ni Oldonyo Morwak, Gombe, Jozani, chwaka bay conservation area, Eastern arc mountains, central slave na ivory trade route,” Alibainisha.
Alifafanua kuwa lengo la mkataba huo ni kuleta uhalali wa orodha ya kidunia katika usawa wa kimazingira na kitamaduni, kuwa na hifadhi sahihi ya maeneo hayo, kutangaza na kujenga uwezo wa kupata misaada, kutoa elimu na uelewa juu ya umuhimu wa kuwa na maeneo hayo pamoja na ushiriki wa jamii katika urithi huo katika usimamizi na utekelezaji wa mkataba huo.
Alieleza kuwa mkataba huo uliridhika na nchi wanachama ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazozuia uendelevu wa maeneo hayo ya urithi pamoja na kuwa kama chombo kinachotoa maelekezo ni kwa namna gani maeneo hayo ya urithi wa asili na kitamaduni yasimamiwe.
Aidha Alieleza changamoto zinazokabili utekelezaji wa mkata huo katika maeneo mbalimbali Duniani ni pamoja na shughuli za kibinadamu katika maeneo ya hifadhi, ucheleweshaji wa malipo ya uwanachama kwa nchi wanachama pamoja na Imani za kijamii za Mila na desturi ambazo hazikubali matokeo ya kisayansi katika utunzaji wa maeneo hayo.
Kwa Upande wake Kamishna msaidizi mwandamizi wa uhifadhi kotoka mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, Mhandisi Joshua Mwankonda alisema kuwa semina hiyo ni muendelezo wa namna ambayo mamlaka hiyo inatoa elimu kwa ukubwa wake wa uhifadhi, maendeleo pamoja na utalii kwa wanahabari ambapo kutokana na maadhisho hayo na mkutano huo wameona ni vema kutoa elimu juu ya mkataba huo wa uridhi wa kidunia ambayo elimu yake na taarifa zake bado zipo chini.
“Ni kuongeza uelewa wa nini maana ya mkataba huo ambao nchi yetu imeridhia na nini katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro kinafanyika katika huu mkataba na kwasasa imekuwa ni agenda kitaifa na kimataifa, kupata wataalamu wengi wa kiafrika ambao watakuwa wanafanya shughuli hizi tofauti na miaka ya nyuma ambayo ilikuwa inaoneka ilikuwa inafanywa na wazungu pekee katika maeneo ya hifadhi na kusimamia mkataba huu na kuhifadhi wa urithi huu kwa kizazi hiki na kizazi kijacho kwa faida za kielimu sayansi na utalii,”Mhandisi Mwankonda.
Hata hivyo zaidi ya wataalamu 50 kutoka nchi mbalimbali Duniani wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo utakaoenda sambamba na maadhisho hayo ambapo Afrika Ina urithi wa kidunia wa asili na kitamaduni 98 sawa na asilimia 8.5, nchi za Uarabuni zikiwa zinazo 88 sawa na asilimia 7.6, Asia na Pacific 277 sawa na asilimia 24.0, Europe na north America 545 sawa na asilimia 47.2, pamoja na Latin America na Caribbean146 sawa na asilimia 12.7 jumla dunia nzima  zikiwa ni 1154 huku maeneo mengine katika nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Tanzania yakisubiri kuingia katika orodha hiyo.

About the author

mzalendoeditor