Featured Kitaifa

WAHITIMU VYUO VIKUU WAASWA KUTUMIA VYEMA ELIMU WANAYOIPATA

Written by mzalendoeditor

Na WyEST
Mwanza

Wahitimu wa Vyuo Vikuu wameaswa kutumia vema elimu wanayopata kuleta tija kwa Taifa.

Hayo yamesemwa Jijini Mwanza na Mhe. Dkt. Phillip Mpango wakati wa mahafali ya 41 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).

Aidha, Mhe. Mpango ameagiza Wizara ya Elimu kuhakikisha vituo vyote vya Chuo hicho vinaunganishwa na mkongo wa Taifa ili kuwezesha matumizi ya TEHAMA na kupunguza gharama za uendeshaji .

“Vituo vyote vya Chuo Kikuu Huria vitaunganishwa na mkongo wa Taifa na hili naagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha linafanyika mara moja ili kupunguza gharama za uendeshaji,” ameongeza Mhe. Mpango

Awali akiongea katika mahafali hayo, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema Chuo Kikuu Huria kimetengewa fedha kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu, kusomesha wahadhiri na miradi mingine.

“Serikali kwa kutambua mchango wa Chuo Kikuu Huria katika kupeleka elimu kwa jamii kupitia mradi wa HEET tutajenga maabara saba katika mikoa ya Njombe, Arusha, Dodoma, Mwanza, Kigoma, Mtwara na Pwani ambazo zitajikita katika tafiti za kisayansi kulingana na shughuli na mahitaji muhimu ya eneo husika,” amefafanua Waziri Mkenda.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa Serikali imetoa zaidi ya Shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya kujenga vituo vya Chuo Kikuu Huria katika mikoa ya Geita, Kigoma, Lindi, Simiyu na Manyara ambao mikoa hii ilikuwa ikitumia majengo ya kukodi kwa gharama kubwa.

Zaidi ya Wahitimu 4,000 wametunukiwa Shahada mbalimbali zikiwemo Shahada Umahiri na Uzamivu wakiwemo wanafunzi kutoka nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Ghana, Malawi, Zambia, Congo, Namibia na Ethiopia.

About the author

mzalendoeditor