Featured Kitaifa

PADRI MINGA AWAFUNDA VIJANA,AWATAKA KUONDOKANA NA ULEVI NA UTUMIAJI WA MADAWA YA KULEVYA

Written by mzalendoeditor

Mratibu wa Utume wa Vijana Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padri Aldolfu Bernard Minga,akitoa Semina  kwa Vijana katika Kongamano la Vijana Wakatoliki Wafanyakazi (VIWAWA) Ngazi ya Kanda,lililofanyika katika Viwanja vya Parokia ya Kanisa Kuu la Kiaskofu la Moyo Mtakatifu wa Yesu-Jimbo Katoliki la Singida

Vijana Wakatoliki Wafanyakazi (VIWAWA wakiwa kwenye Semina iliyofanyika katika Viwanja vya Parokia ya Kanisa Kuu la Kiaskofu la Moyo Mtakatifu wa Yesu-Jimbo Katoliki la Singida. .(Picha zote na Ndahani Lugunya).

………………………………………….

Na Ndahani Lugunya,Singida.

IMEELEZWA kwamba Kijana mzuri ni yule aliyetengenezwa vizuri katika utoto wake,kwani mtoto akilelewa katika mazingira na Malezi mabovu hata ujana wake utakuwa mbovu.

Hayo yameelezwa na Mratibu wa Utume wa Vijana Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padri Aldolfu Bernard Minga, wakati akiwasilisha Mada yake inayohusu “Nafasi ya Kijana katika Kanisa”,katika Kongamano la Vijana Wakatoliki Wafanyakazi (VIWAWA) Ngazi ya Kanda,lililofanyika katika Viwanja vya Parokia ya Kanisa Kuu la Kiaskofu la Moyo Mtakatifu wa Yesu-Jimbo Katoliki la Singida.

Padri Minga amesema kwamba Kijana ni nguzo ya Kanisa katika imani,maadili,Sala,usomaji wa Neno la Mungu,Uchumi na Uongozi,huku akiongeza kuwa suala la umri lisimtafsiri Kijana kwani wapo baadhi yao wamejitumbukiza katika ulevi,lishe duni na utumiaji wa madawa ya kulevya na hivyo kuwafanya waonekane Wazee katika jamii tofauti na umri wao.

“Leo hii unakutana na Kijana mwenyewe umri wa miaka 18 lakini ukimuangalia mwonekano wake ni kama Mzee wa miaka 50,Kwa sababu anakuwa kachoka na hii ni kutokana na utumiaji wa madawa ya kulevya na unywaji wa pombe uliopitiliza” amesema Padri Minga.

Aidha Padri Minga amesema kwamba katika umri wa Kijana kuna mambo msingi yanayopaswa kuangaliwa kwa umakini na kwa ungalifu mkubwa,ambapo katika umri wa miaka 15-45 Kijana afundishwe na kutayarishwa namna ya kutoa maamuzi,namna ya kuacha umaskini na mila potofu na kuishi vizuri Ukristo wake.

“Wapo Vijana wengine wameshindwa kuwa na mamuzi sahahi katika maisha yao,yaani hata akigombana na mke au mume wake anakimbilia nyumbani kwa wazazi wake ndiyo wakatoe maamuzi.kuomba ushauri sio jambo baya lakini nawewe jifunze kuwa mtu wa maamuzi katika mambo yako na huo ndio ukomavu wa Kijana,” amesisitiza Padri Minga. 

Amesema Dunia ya leo na kesho inawategemea Vijana,ndiyo maana Kanisa Katoliki Ulimwenguni pia limewekeza Nguvu kubwa katika malezi adilifu  ya Kiroho na Kimwili kwao kwa sababu Vijana ni tunu,hazina na thamani katika Kanisa .

Katika hatua nyingine Padri Minga ametoa wito kwa Vijana kuwa faraja kwa wengine na si kuwakatisha tama.

Amewataka vijana kuwa makini na mawazo na ushauri wanaopewa na watu mbalimbali,kwa kuyachambua na kuona yanastahili kufanyiwa kazi au la kwani yapo baadhi ya mawazo huwa ni ya kukatisha tama katika kukua kiuchumi na kiroho.

Pamoja na hilo amesema kwamba Kijana Mkatoliki anapaswa kuweka kipaumbele mambo makuu manne katika maisha yake ya kila siku,ambapo mambo hayo ni Imani,Uchumi,Siasa na fani mbalimbali na kuongeza kuwa,Kijana ni lazima awe sehemu ya amani popote pale anapokuepo.

Aidha Padri Minga amesema kwamba Kijana anapaswa kuwa mtu mwenye majibu mengi na si kuwa mtu mwenye maswali mengi,kwani Kanisa na Taifa linahitaji vijana imara wenye umakini katika maamuzi.

Kongamano hilo la Siku 7 lililofunguliwa na Makamu wa Askofu wa Jimbo la Singida Padri Francis Limu,limewajumuisha jumla ya Vijana 464 ambapo miongoni mwao 447 ni kutoka Jimbo Katoliki Singida na 17 kutoka Jimbo Katoliki Kondoa,kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni yaliyofikia kilele chake Dominika ya 34 mwaka C wa Kanisa Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme.

About the author

mzalendoeditor