Featured Kitaifa

MAKAMU WA RAIS ATETA NA WANANCHI MKATA TANGA

Written by mzalendoeditor

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza na viongozi pamoja na wananchi mbalimbali katika eneo la Mkata Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wakati akiwa njiani kuelekea makao makuu ya mkoa huo kwaajili ya ziara ya kikazi

  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza na viongozi pamoja na wananchi mbalimbali katika eneo la Mkata Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wakati akiwa njiani kuelekea makao makuu ya mkoa huo kwaajili ya ziara ya kikazi leo tarehe 19 Novemba 2022.

………………………..

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa siku saba kwa Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha wanatatua changamoto inayokwamisha ujenzi wa barabara ya Pangani – Makurunge Bagamoyo ambayo imekwama kutokana na eneo la jiwe la kuchimba kokoto leseni yake ya uchimbaji kupewa mtu mwingine tofauti na mkandarasi husika.

Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 19 Novemba 2022 wakati aliposimama kuzungumza na wananchi wa Mkata Wilaya ya Handeni mkoani Tanga akiwa njiani kuelekea makao makuu ya mkoa huo kwaajili ya ziara.

Ameagiza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuhakikisha wanafanyia kazi mapema zaidi maeneo yanayotumika kwaajili ya ujenzi wanayoyapata baada ya tafiti wanazofanya ili kuepusha migogoro inayokwamisha maendeleo ya miradi.

Pia ameagiza kutatuliwa mara moja changamoto iliokwamisha ujenzi wa barabara ya Handeni – Kibirashi – Kiteto hadi Dodoma ambayo ujenzi wake ulipaswa kuanza tangu mwezi Mei mwaka huu.

Halikadhalika Makamu wa Rais ameagiza uongozi wa mkoa wa Tanga kuhakikisha wanafanya vikao na wafugaji kwa lengo la kuwapa elimu ya sheria na taratibu za nchi ili kuondokana na migogoro inasababishwa na wafugaji kulisha mifugo katika mashamba ya wakulima.

Pia Makamu wa Rais ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama wilayani Handeni kufuatilia na kuwachukulia hatua wafugaji waliowajeruhi wakulima wakiwa mashambani ili kulinda amani iliopo nchini.

Aidha ametoa wito kwa wakulima kutochukua sheria mkononi wakati wote migogoro baina yao na wafugaji inapojitokeza.Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Mkata na Tanga kwa ujumla kuongeza jitihada katika utunzaji wa mazingira ikiwemo upandaji miti ili kuepukana na changamoto za ukame zinazojitokeza hivi sasa.

Pia amewaasa wazazi na walezi mkoani humo kuhakikisha wanatumia vema fursa ya elimu inayotolewa bila malipo na serikali kwa kuwapeleka Watoto wao kupata elimu kwa maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omary Mgumba amesema mkoa huo utaendelea kusimamia uhifadhi wa mazingira kwa kuchukua hatua kali zaidi ili kukabiliana na waharibifu.

Amesema mkoa huo kwa sasa unakabiliwa na changamoto ya ukataji miti kwaajili ya uchomaji mkaa na baadhi ya viongozi katika maeneo ya vijiji na vitongoji wakishiriki katika biashara.

About the author

mzalendoeditor