Featured Kitaifa

WAZIRI STERGOMENA TAX AIPONGEZA SERIKALI YA UAE KWA KUFUNGUA UBALOZI MDOGO ZANZIBAR

Written by mzalendoeditor

p>

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt.
Stergomena  Tax amepongeza uamuzi wa Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu
(UAE) wa kufungua Konseli Kuu (Ubalozi Mdogo) Visiwani Zanzibar na kutoa wito
kwa Wananchi kutumia uwepo wa Konseli hiyo kuboresha ushirikiano katika sekta
mbalimbali zikiwemo biashara, utalii na masoko kwa bidhaa za Tanzania.

 

Mhe. Dkt. Tax ametoa pongezi hizo hivi karibuni wakati akipokea Hati za
Utambulisho za Konseli Mkuu wa UAE, Zanzibar   Mhe. Balozi Saleh Ahmed
Alhemeiri katika hafla fupi iliyofanyika katika Ofisi za Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Zanzibar.

 

Amesema hatua hiyo ni muhimu sana katika kuimarisha ushirikiano wa
kihistoria uliopo kati ya Tanzania na UAE kwani  sasa fursa nyingi
zilizopo Zanzibar ikiwemo utalii, uchumi wa buluu na biashara vitashamiri zaidi
na kukua.



Ameongeza kusema Serikali ya Awamu ya Sita chini
ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na Serikali  ya Awamu ya Nane ya Zanzibar chini ya uongozi wa Mhe. Dkt.
Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  zimeendelea kuimarisha ushirikiano na nchi
mbalimbali pamoja na kutafuta fursa za biashara, utalii, uwekezaji  na
masoko kwa bidhaa za Tanzania ili kuiwainua kiuchumi watanzania wote.

 

Ameongeza kwamba kufunguliwa kwa Konseli Kuu hiyo ni matokeo ya
ziara mbalimbali za viongozi hao nchini humo ikiwemo ile ya Mhe. Rais Samia
aliyoifanya nchini UAE mwezi Februari 2022 wakati wa Maonesho ya Biashara ya
Kimataifa ya Dubai Expo 2020.

 

Pia amesema wakati wa ziara hiyo, pamoja na mambo mengine,
Mikataba na Hati za Makubaliano mbalimbali  zilisainiwa kwa ajili ya
kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.

 

“Napongeza kwa dhati uamuzi wa Serikali ya UAE wa kufungua Konseli
Kuu au Ubalozi mdogo hapa Zanzibar. Ni imani yangu kuwa, uwepo wa Konseli Kuu
hii utasaidia kuharakisha utekelezaji wa masuala mbalimbali ya
ushirikiano ambayo tayari yamekubalika kwa manufaa ya pande hizi mbili”
alisema Dkt. Tax.

 

Akitaja maeneo ya kipaumbele ya ushirikiano kwa upande wa Zanzibar, Mhe.
Waziri Tax amesema ni pamoja na Uchumi wa Buluu hususan katika uvuvi wa bahari
kuu, utalii, biashara na uwekezaji kwa ujumla
.



Pia Mhe. Dkt Tax amemhakikishia ushirikiano Balozi
huyo na kwamba ana imani kuwa kupitia yeye masuala mengi yatakamilika.

 

” Tutashirikiana na wewe kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa kati
ya nchi hizi mbili hususan kwa upande wa Zanzibar yanatekelezwa na kama
ulivyosema awali kwa kiasi fulani Zanzibar inafanana na Dubai, basi tujielekeze
kuigeuza  Zanzibar  kuwa  Dubai ya Afrika” alisema Dkt. Tax.

 

Kwa upande wake, Mhe.  Alhemeiri amesema amefarijika kuwepo
Zanzibar na kwamba yupo tayari kushirikiana na Serikali hiyo katika kukuza
biashara, kilimo, elimu, na uchumi wa buluu kwani zipo fursa lukuki katika
Kisiwa hiki zinazohitaji kuendelezwa.

 

“Nia yetu ni kushirikiana na Serikali kukiendeleza Kisiwa kizuri
cha  Zanzibar. Nimeona zipo fursa nyingi
za kufanyia kazi. Nitajikita zaidi kwenye masuala ya utalii, biashara, elimu,
uchumi wa buluu na usafirishaji kwa kuzishawishi mamlaka za UAE kuongeza safari
za moja kwa moja za Mashirika ya Ndege ya UAE kuja Zanzibar ili kukuza utalii,
alisema Mhe. Alhemeiri. 



Mhe. Dkt. Tax yupo mjini Zanzibar kwa ajili ya
kushiriki Mkutano wa Sita wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Samia Suluhu Hassan na Mabalozi wa Tanzania unaofanyika Kisiwanio humo kuanzia
tarehe 14 hadi 21 Novemba 2022. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akipokea hati za utambulisho kutoka kwa Konseli Mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Visiwani Zanzibar, Mhe. Balozi Saleh Ahmed Alhemeiri. Hafla hiyo fupi imefanyika hivi karibuni katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Zanzibar. Mhe. Dkt. Tax yupo mjini Zanzibar kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Sita wa Mabalozi wa Tanzania unaoendelea mjini hapo kuanzia tarehe 14 hadi 21 Novemba 2022
 
Mhe. Dkt. Tax akizungumza na Mhe. Alhemeiri mara baada ya kupokea hati za utambulisho. Katika mazungumzo hayo, Mhe. Dkt. Tax alipongeza uamuzi wa Serikali wa kufungua Konseli Kuu Zanzibar na kutoa wito kwa watanzania kutumia uwepo wa Ofisi hiyo kuimarisha ushirikiano
 
Mhe. Dkt. Tax akiagana na Mhe. Alhemeiri mara baada ya kumaliza mazungumzo.

 

Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Alhemeiri wakiwa kati picha ya pamoja
Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Alhemeiri wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemed Mgaza (kulia) na Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mariam Mrisho (kushoto)

 

Picha ya pamoja

 

 

 

 

 

 

 

About the author

mzalendoeditor