Featured Kitaifa

”WOTE WALIOVAMIA VYANZO VYA MAJI WAONDOKE MARA MOJA”-WAZIRI JAFO

Written by mzalendoeditor

Na. Jacob Kasiri -Ruaha.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Dkt.
Selemani Jafo (Mb) amewataka wananchi wote waliovamia bonde la Ihefu
ambalo ni chanzo cha mto Ruaha Mkuu kuondoka mara moja ili kuondokana na
athari zilizopelekea mto Ruaha Mkuu kutotiririsha maji kwa miezi mitatu
mfululizo.

Ameyasema hayo leo katika kikao kilichowahusisha
Mawaziri nane wa Kisekta, Makatibu wakuu, wakuu wa Mikoa pamoja na
wataalam kilichofanyika katika Hifadhi ya Taifa Ruaha iliyoko mkoani
Iringa.

“Wale wote waliovamia vyanzo vya maji tumeazimia
waondoke haraka iwezekanavyo, swala la kuondoka halina mjadala wa
kusubiri mwezi au miezi miwili. Mara baada ya kikao hiki cha leo Novemba
15, 2022 wote waliovamia vyanzo vya maji na kusababisha uharibifu
mkubwa mnatakiwa kuondoka mara moja. Hii kauli tukisema mara moja ni
kuanzia leo,” amesisitiza Waziri huyo.

Waziri Jafo ametaja
sababu za kukauka kwa mto Ruaha Mkuu ni pamoja na uingizaji wa mifugo
ndani ya bonde la Usangu na kwenye ardhi oevu ya Ihefu, uchepushaji wa
maji toka kwenye mito inayoingiza maji bonde la Usangu unaofanywa na
baadhi ya wakulima wasiofuata sheria na taratibu pamoja na ukataji na
uchomaji wa misitu unaosababisha ukame na uharibifu wa mazingira.

Eneo
la darajani ambalo Mawaziri, wakuu wa Mikoa na wataalamu hao
wamelitembelea ni moja ya kivutio ndani ya hifadhi hii pindi mto Ruaha
Mkuu unapokuwa unatiririsha maji yake ambapo watalii hushuka na kupiga
picha mbalimbali kutokana na mandhari nzuri ya beta (meanders) za mto
huo, sasa hivi yamesalia madimbwi yenye maji machache na machafu
yanayopelekea maisha ya viboko, mamba, samaki na wanyama wengine
wanaotegemea maji hayo kuwa hatarini.

“Mambo ya haraka ili
kunusuru hali hii ni pamoja na Mamlaka ya bonde za maji kusimamia sheria
iliyopitishwa na Bunge 2022 inayoelekeza wale wote wanaochepusha maji
kinyume cha sheria kuchukuliwa hatua. Pia naelekeza Mamlaka ya bonde za
maji pamoja na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira
(NEMC) kubaini wale wote waliovamia vyanzo vya maji waondoke haraka”,
aliongeza Waziri huyo.

Uhai wa hifadhi ya taifa Ruaha hutegemea
mto Ruaha Mkuu, hivyo kukauka kwake hakutaathiri tu hifadhi hii katika
shughuli za utalii na uhifadhi bali pia itaathiri shughuli za kiuchumi
kama vile uzalishaji wa umeme, kilimo na uvuvi unaofanyika katika bwawa
la Mtera. Kama tujuavyo zaidi ya asilimia 65 ya umeme unaozalishwa kwa
njia ya maji nchini Tanzania hutegemea maji yanayotokea bonde la Ihefu
kupitia mto Ruaha Mkuu.

About the author

mzalendoeditor