Featured Kitaifa

RC MWASA AITAKA MORUWASA KUJENGA UZIO BWAWA LA MINDU

Written by mzalendoeditor

NA FARIDA MANGUBE, MOROGORO.

MKUU wa mkoa wa Morogoro Fatma Mwasa ameiagiza mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Moruwasa ,  kujenga uzio katika bwawa la Mindu  lililopo manispaa ya Morogoro, ili kudhibiti shughuli za kibinadamu zinazoendelea kufanyika kando mwa bwawa hilo ikiwemo kilimo.

Mkuu huyo wa mkoa alitoa agizo hilo wakati wa kikao cha pamoja na wadau wa maji cha kujadili mikakati mbalimbali itakayosaidia kuondoa tatizo la maji mkoani humo.

“Kuzunguka bwawa la Mindu hakuna mtu yoyote atakayeruhusiwa kufanya shughuli za kibinadamu, tunaweka uzio “alisema.

Alisema bwawa hilo linategemewa kwaajili ya maji kwa matumizi ya binadamu kwa miaka 50,000 ijayo, hivyo upo umuhimu mkubwa wa kulihifadhi na kulitunza.

Pia alisema wataweka mabango makubwa nyenye zuio la mtu yoyote kuingia katika bwawa hilo, sambamba na kurejesha uoto wa asili kwa kupanda miti zaidi katika bwawa hilo

Chifu wa kabila la Waluguru Kingalu Mwana Banzi wa 15 akizingumza na waandishi wa habari, alisema  hali ya vyanzo vya maji siyo nzuri kwa sasa na kuiomba serikali na wadau mbalimbali kuungana na machifu kwaajili ya kunusuru hali hiyo.

“Sisi machifu tunauwezo wa kuombea mvua ikanyesha na pia tunaweza kuzuia majanga mbalimbali kwa kutumia mila na desturi zetu”alisema.

Alisema tangu enzi za baba wa Taifa Mila na desturi zilitumika katika kuombea mvua na majanga mengine, hivyo sio jambo geni kwa Watanzania hivyo ni muhimu likaendelea kupewa nafasi 

Pia aliomba Rais Samia Hassan Suluhu kutumia rungu lake kuzuia mashine za kukata miti maarufu kama chenso ambazo zimekuwa kisababishi kikubwa cha ukataji miti hovyo na hivyo kuharibu mazingira na kusababisha kukosekana kwa mvua.

“Chenso nitatizo kubwa, nameomba Rais Samia atoe zuio ili zisitumike kupunguza huu uharibifu wa mazingira.

Pia aliomba serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza bei ya bidhaa za chuma ili watengenezaji wa bidhaa za miti wawe na mbadala huo.

“Naomba Serikali iangalie uwezekano pia wa kupunguza gharama za gesi ili watu watumie gasi badala ya mkaa”alisema.

About the author

mzalendoeditor