Featured Kitaifa

MBUNGE CHIKOTA ATAKA PEMBEJEO ZA KOROSHO ZITOLEWE KWA WAKATI

Written by mzalendoeditor

Mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota amehoji mpango wa serikali wa kuhakikisha pembejeo za korosho kwa msimu wa mwaka 2022/23 zinapatikana kwa wakati na kwa bei nafuu.

Akiuliza maswali bungeni leo, Chikota, amesema kwa miaka miwili mfululizo serikali imekuwa ikiahidi viuatilifu lakini kiasi kinachotolewa na usambazaji hakiendani na kilichoahidiwa na kusababisha upungufu wa pembejeo kwa wakulima.

“Serikali inatoa kauli gani kuhusu pembejeo za unga na dawa za maji zitapatikana kwa wakati na kufika kwa wakulima,”amehoji.

Pia ametaka serikali kuhakikisha ongezeko la uzalishaji korosho litaendana na bei yenye tija kwa mkulima kwa kuwa kwasasa

kwenye minada ya korosho bei inaendelea kuporomoka.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde, amesema mahitaji ya pembejeo za zao la korosho katika msimu wa 2023/2024 ni tani 70,000 za salfa ya unga na lita milioni 3.4 za viuatilifu vya maji, mabomba 10,000 na magunia milioni 6.2.

Amesema miongoni mwa mikakati ya kukabiliana na kuporomoka kwa bei ya korosho nchini ni kuwezesha wabanguaji wadogo wa korosho ghafi.

Amebainisha hivi sasa wanaendelea kutafuta masoko nje ya nchi na wiki iliyopita alikwenda uwanja wa ndege kusindikiza kontena la korosho zilizobanguliwa ambapo soko limepatikana Marekani na kilo moja inauzwa Sh.90,000.

“Hivyo mkakati wa serikali ni kuwawezesha wabanguaji wadogo ili tuachane na soko la Vietnam na India ambapo kumekuwa na changamoto kubwa ya bei,”amesema.

Amesisitiza serikali itasimamia kuhakikisha viuatilifu hivyo vinafika kwa wakati na kuondoa kero zilizowakumba misimu iliyopita.

Amesema Wizara kupitia Bodi ya Korosho Tanzania inasimamia upatikanaji wa pembejeo za korosho kabla ya msimu kuanza ambapo Oktoba 15,2022, kamati ya ununuzi wa pembejeo kwa pamoja ilisaini mikataba na kampuni 14 kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo hizo.

“Serikali kupitia Bodi ya Korosho Tanzania inaendelea kuratibu zoezi hilo ili kuhakikisha kuwa pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati na bei itakayopangwa kulingana na mahitaji,”amesema.

About the author

mzalendoeditor