Featured Michezo

GEKUL AIPONGEZA GEITA MJI UJENZI WA UWANJA

Written by mzalendoeditor

Na Shamimu Nyaki – Dodoma

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul ametoa pongezi kwa Halmashauri ya Geita Mji kwa ujenzi wa Uwanja wa mpira wa Miguu ambao umefikia asilimia 75.

Naibu Waziri Gekul, ametoa pongezi hizo leo Novemba 7, 2022 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Geita Mjini Mhe.Costantine John Kanyasu, aliyeuliza kuhusu mchango wa Serikali katika ujenzi wa uwanja wa kisasa wa michezo wa Halmashauri ya Geita Mji.

“Kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Taifa ya Mwaka 1995 Ibara ya 7(i- iv), jukumu la ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya michezo ni jukumu la serikali kuu, Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na wadau wa Sekta ya Michezo, hivyo natoa wito kwa Halmashauri zote nchini kuiga mfano wa Geita Mji” alisema Mhe. Gekul

Mhe. Gekul ameongeza kuwa, wizara yake inatoa ushauri wa kitaalamu katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya michezo pale inapohitajika kama ilivyofanya katika Halmashauri ya Chalinze, Tunduma na Ruangwa pamoja na Taasisi za Bandari na Gymkana.

Akijibu maswali ya nyongeza ya Mhe. Kanyasu kuhusu mpango wa haraka wa kukuza michezo na kusaidia timu za Taifa na kiasi cha fedha kilichopelekwa Geita kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo, Naibu Waziri Mhe.Gekul, ameleza kuwa, Serikali inaendelea kuwekeza katika timu za Taifa na tayari kupitia uwekezaji huo matokeo yanaonekana kwa baadhi ya timu.

Aidha, Mhe. Gekul amesema kuwa kiasi cha shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya Chuo Cha Michezo Malya ambacho kinazalisha wataalamu wa michezo huku kiasi cha shilingi Bilioni 2 zimetengwa kwa ajili ya akademi za michezo katika shule zilizotengwa pamoja na shilingi Bilioni 7 za kukarabati viwanja vya michezo ikiwemo Arusha, Mbeya na Dodoma.

About the author

mzalendoeditor