Featured Kitaifa

TANKI LITA MILIONI MOJA KUMALIZA TATIZO LA MAJI MUHIMBILI

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (MB) akikisitiza jambo katika kikao maalumu ya kuangalia hali ya upatikanaji maji Hospitali ya Taifa Muhimbii

………………………………….

Wizara ya Maji kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) itafunga tanki la maji Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH-Upanga) lenye ujazo wa lita za maji milioni moja ili kukabili tatizo hilo ambalo litagharimu TZS. 500 Mil.

 

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (MB) alipotembelea MNH ili kuona changamoto ya maji iliyopo hususani kwa wagonjwa wanaosafisha damu ambao maji yanayotumika kwenye mfumo wa mashine yanatakiwa kutoka DAWASA na siyo ya visima.

 

Akitoa taarifa kuhusu tatizo la maji, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Mohamed Janabi, amesema kwa upande wa Upanga hospitali inatumia lita 1,500,000 kwa siku na kiasi cha maji yanayotoka DAWASA kabla ya uhaba wa maji ilikua kati ya lita 850,000 kutoka Ruvu Juu na Ruvu Chini na sasa kiasi hicho kimepungua kufikia lita 400,000 kwa siku hali iliyoleta athari katika utoaji huduma. Hata hivyo hospitali inatumia maji ya visima kufidia upungufu huo isipokuwa tu wagonjwa wanaosafishwa figo.

 

Maji yanayotoka Ruvu Chini husambazwa Jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD) lita 70,000 na Jengo la Watoto lenye Kitengo chenye huduma za kusafisha damu hutumia lita 60,000 za maji kwa siku hivyo kutokuwa na maji huduma zimeathiri kwa baadhi ya wagonjwa kusogezwa siku moja zaidi katika mzunguko wake.

 

Prof. Janabi amesema MNH ina mashine 42 za kusafisha damu na zote zinafanya kazi. Huduma hutolewa kwa awamu tatu kwa siku kuanzia saa 10 alfajiri hadi saa mbili asubuhi, saa 03:00 asubuhi hadi saa 08:30 mchana na awamu ya tatu ni kuanzia saa 09:30 mchana hadi 01:30 jioni ambapo wastani wa wagonjwa ni 100 kwa siku  na kwa mwezi wagonjwa 2,860.

 

Katika hatua nyingine, Mhe. Aweso ameiagiza DAWASA kuhakikisha inaleta ufumbuzi wa kudumu wa kutatua changamoto ya maji ikiwemo kutoa magari ya maji yenye ujazo wa lita 18,000 na 10,000 kusambaza maji katika kitengo hicho ili wagonjwa wa figo waweze kupata huduma.

 

“Nawaagiza DAWASA kuhakikisha leo wanaleta timu ya watalaamu ili ishirikiane na watalaamu wa MNH kufanya mpango wa kuchepusha maji yanayotoka njia ya Ruvu Juu yaweze kusambazwa kitengo cha kusafisha damu ambacho hupata maji kupitia njia ya Ruvu Chini ili kuondoa tatizo hilo mara moja” amesisitiza Mhe. Aweso.

 

Kaitka hatua nyingine Mhe. Aweso amemuagiza Mkurugenzi wa Bodi ya Maji ya Bonde la Wami-Ruvu, Mhandisi Elibariki Mmasi kuanza mara moja upembuzi wa kuchimba kisima kikubwa cha maji ndani ya MNH ili kuipa vyanzo vya kutosha vya maji katika kipindi chote cha mwaka.

 

Ziara hii ilimshirikisha Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi ambaye kwa upande wake amemshukuru Mhe. Aweso kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (MB) kwa namna ambavyo ameitikia haraka na kufika eneo la MNH ili kuona namna ya kutatua tatizo la maji.

 

Prof. Makubi ametumia fursa hiyo kuzitaka hospitali zote nchini kuhakikisha zinakua na njia mbadala katika kutekeleza majukumu yake pindi inapotokea changamoto ama ya umeme au maji.

 

Pia Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Antony Sanga amemuahidi Mhe. Aweso kusimamia maagizo yote aliyotoa kwa Wizara yake ili yaweze kutekelezwa kikamilifu.

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (MB) akikisitiza jambo katika kikao maalumu ya kuangalia hali ya upatikanaji maji Hospitali ya Taifa Muhimbii

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi akieleza kuhusu hali ya upatikaji maji 

Baadhi ya Viongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili  wakisikiliza maelekezo mbalimbali.

Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi akizungumza katika kikao hicho.

Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mhandisi. Anthony Sanga akifafanua jambo katika kikao hicho.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi (kushoto) akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi baada ya

Waziri wa Maji Mhe. Aweso katika picha ya pamoja na Viongozi wote walioshiriki kikao hicho

About the author

mzalendoeditor