Featured Kitaifa

SERIKALI YATOA TAMKO MKUTANO WA MABADILIKO YA TABIANCHI

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akitoa tamko Serikali Kuhusu Msimamo wa Tanzania kwenye Majadiliano ya Mkutano wa 27 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi Utakaofanyika Tarehe 7-18 Novemba 2022 Jijini Sharm El-Sheikh, Misri. Waziri Jafo ametoa tamko hilo tarehe 2 Novemba, 2022 Jijini Dar es Salaam.

……………………………

WAZIRI  wa Nchi Ofisi ya Makamu (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amesema Tanzania imejiandaa kikamilifu kushiriki Mkutano wa 27 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi utakaofanyika Sharm El Sheikh nchini Misri kuanzia tarehe 31 Oktoba mpaka tarehe 18 Novemba 2022.

Amesema katika Mkutano wa mwaka huu, majadiliano yenye maslahi mapana kwa nchi yetu yatapewa kipaumbele na kuweka msimamo katika Malengo ya Dunia juu ya Uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Jafo amesema kuwa agenda ya mabadiliko ya tabianchi ndio kipaumbele cha nchi zinazoendelea na kusema kuwa umeanzishwa mkakati wa kidunia wa uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi. “Inakadiriwa kuwa takribani zaidi watu bilioni 3.6 wako katika hatari ya kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi. Hivyo, lengo la dunia kwa pamoja ni kutaka kuondokana na hali hii” Jafo alisisitiza.

Amesema masuala ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabianchi yataendelea kuwa sehemu kubwa ya majadiliano kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea. Amesisitiza kuwa agenda kubwa itakuwa ni upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya mabadiliko ya tabianchi.

Amesema kuwa msimamo wa Tanzania katika mkutana huo ni kutoa wito kwa nchi zilizondelea kutimiza wajibu wao ili kuwezesha uhakika na uwazi wa upatikanaji wa fedha za mabadiliko ya tabianchi.

Tanzania inasisitiza kuwekwa kwa mfuko maalum kwa ajili ya kushughulikia masuala ya hasara na uharibifu ili kusaidia nchi zinazoendelea kufanya tathmini ya kuongezeka kwa kina cha bahari na Upunguzaji wa gesijoto chini ya mkataba na makubaliano ya Paris kwa nchi zinazoendelea na kuchangia shughuli za maendeleo.

Kuhusu Masoko ya kaboni na mbinu zisizo za masoko, Dkt. Jafo amesema kuwa Msimamo wa Tanzania ni udhibiti wa matumizi ya masoko ya kaboni katika upunguzaji wa gesijoto ili kuzifanya nchi zilizoendelea kuchukua hatua za ndani kushughulikia upunguzaji wa uzalishaji wa gesijoto.

Ameyataja mambo mengine yatakayojadiliwa kuwa ni pamoja na Mfumo wa uwazi katika hatua na misaada inayotolewa kwa kuzingatia fedha za misaada zinazotolewa, kujenga uwezo na teknolojia.

“Tunasisitiza kuwa hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zisiathiri juhudi za kijamii na kiuchumi za nchi zinazoendelea na hazipaswi kuwa njia ya ubaguzi wa kiholela, usio na sababu au kizuizi cha kujificha kwenye biashara ya kimataifa, haswa kikanda” Dkt. Jafo alisisitiza.

Itakumbukwa kuwa, katika mkutano wa 26 wa nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika tarehe 31 Oktoba 12 Novemba 2021, huko Glasgow, Uskochi, Uingereza, Tanzania imeendelea kutekeleza na kuchukua hatua muhimu ikiwemo kuandaa Mpango wa Kuhuisha masuala ya kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi katika Sera, Mipango, Mikakati na Programu za nchi.

Amesema kuwa Serikali imeandaa Mpango Kabambe wa Hifadhi ya Mazingira wa mwaka 2022-2032 ambao unabainisha masuala ya vipaumbele ya usimamizi wa Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi na kuanzisha majadiliano na Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund) na mifuko mingine kwa lengo la kupata fedha za kusaidia kuandaa na kutekeleza Miradi ya Taifa ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi
Mwaka huu Tanzania inashiriki kitofauti ambapo kutakuwa na Banda la Tanzania la Maonesho ambalo litaonesha hatua/jitihada mbalimbali katika sekta tofauti.

“Katika banda letu tutaionyesha jumuiya ya kimataifa mambo tuliyoyafanya kuanzia undaaji wa Sera, Miongozo na mikakati mbalimbali pamoja na miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa ili kukabiliana au kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi” Dkt. Jafo alisisitiza.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi mwanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi ulioridhiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Aprili mwaka 1996. Lengo kuu la Mkataba huu ni kuhakikisha kuwa mlundikano wa gesijoto angani zinazosababishwa na shughuli za binadamu unadhibitiwa bila ya kuleta madhara kwa binadamu na mazingira

About the author

mzalendoeditor