Featured Kitaifa

MAKAMPUNI KUSHINDANISHWA KWENYE UBORA WA BIDHAA NA HUDUMA

Written by mzalendoeditor

MWAKILISHI wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji,Viwanda na Biashara,Aristides Mbwasi,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa kuhusu tuzo za ubora za kitaifa kwa mwaka 2022-2023 leo Oktoba 27,2022 jijini Dodoma.

……………………………………

Na Alex Sonna-DODOMA

SERIKALI imezindua mashindano ya tuzo za ubora kwenye huduma na  bidhaa  zenye lengo la kuhakikisha mifumo,bidhaa na huduma zinakidhi ubora kitaifa,kikanda na kimataifa ili kufanya vizuri kwenye masoko ya ngazi zote.

Tuzo hizo ambazo zitakuwa katika vipengele vitano ni pamoja na  kwa kampuni bora ya mwaka,bidhaa bora ya mwaka,huduma bora ya mwaka,muuzaji bora wa bidhaa nje ya nchi na mtu mmoja mmoja aliyefanya vizuri kwenye masuala ya bora.

Hayo yameelezwa leo Oktoba 27,2022 Jijini Dodoma na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji,Viwanda na Biashara,Aristides Mbwasi wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu tuzo za ubora za kitaifa kwa mwaka 2022-2023.

Mbwasi amesema tuzo za ubora zilianzishwa ikiwa ni makubaliano baina ya wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ili kutambua na kukuza sekta ya biashara kupitia ubora wa biadhaa na huduma katika ukanda huo.

“Kwa sababu hiyo.serikali kupitia Wizara ya Uwezekezaji,Viwanda na Biashara iliona umuhimu wa kuanzisha tuzo za ubora za kitaifa na kutoa jukumu kuziratibu kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS)

“Kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSP) Taasisi za Viwango Zanzibar (ZBS) Shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo nchini (SIDO) Chama cha Wanawake wafanyabiashara Tanzania (TCCIA) na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade).

Amesema tuzo hizo ni sehemu ya mipango ya serikali katika kuboresha huduma na bidhaa zinazotengenezwa nchini kupitia matumizi ya viwango na kanuni za ubora kwa taasisi za umma na binafsi.

Amesema lengo ni kuhakikisha kuwa mifumo bidhaa na huduma zinakidhi ubora kitaifa,kikanda na kimataifa na hivyo kufanya vizuri kwenye masoko ya ngazi zote.

Mbwasi amesema tuzo hizo zimegawanyika katika vipengele vitano ambavyo ni Tuzo kwa kampuni bora ya mwaka,tuzo kwa bidhaa bora ya mwaka,tuzo huduma bora ya mwaka,tuzo kwa muuzaji bora wa bidhaa nje ya nchi na mtu mmoja mmoja aliyefanya vizuri kwenye masuala ya bora.

“Kwa kipengele cha kwanza hadi cha nne zimeandaliwa tuzo kwenmye makundi mawili kwa kila kipengele yaani tuzo kwa kampuni kubwa na pia tuzo kwa wajasiriamali wadogo na wakati.

Aidha kipengele cha tano kinahusisha tuzo kwa mtu mmoja pekee ambaye atakuwa ni yule aliyefanya vizuri kwenye masuala ya ubora.

Amesema washindi si tu watapata nafasi ya kufahamika pia watapata fursa ya kushiriki kwenye mashindano ya tuzo za ubora kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na pia katika mashindano ya tuo za ubora za nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Mbwasi amesema washindi wa tuzo za ubora mwaka uliopita walishiriki katika mashindano ya kikanda katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Qualty Award) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC Qualty Award.

“Katika mashindano hayo kampuni kutoka Tanzania zilizonyakua tuzo ni Kampuni kubwa bora ya mwaka EAC Said Salim Bakhresa Company Limited,bidhaa bora ya mwaka EAC Faima Production na huduma bora ya mwaka kwa SME EAC –Caps Tanzania Ltd.

“Mataukio haya ni makubwa na yanatoa fursa kwa bidhaa na huduma zinazotolewa hapa nchini kuaminiwa zaidi hata nje ya mipaka ya Tanzania hivyo kupanua wigo wa masoko kwa bidhaa na huduma,”amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Shirika la viwango Tanzania (TBS) Dkt Yusuph Ngenya,amesema kuwa maandalizi  yanaendelea vizuri kwa kutumia warsha mbalimbali na vyombo vya habari ,mitandao ya kijamii ambapo yatasaidia kuwapata washindi.

“Katika maandalizi haya tumewapa kipaumbele akina mama wajasiliamali kuwahamasisha ili waweze kushiriki kwani ni wengi ambao wamejikita kwenye ujasiliamali.” amesema Ngenya.

Naye  Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Viwango ambaye amemwakilisha Mkrugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS)Bi.Hafsa Ali Slim,amesema kuwa wanatarajia kutoa uelewa kwa wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa mbalimbali kwa upande wa Zanzibar ili waweze kushiriki kwa wingi zaidi.

MWAKILISHI wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji,Viwanda na Biashara,Aristides Mbwasi,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa kuhusu tuzo za ubora za kitaifa kwa mwaka 2022-2023 leo Oktoba 27,2022 jijini Dodoma.Kulia ni Mkurugenzi Mkuu Shirika la viwango Tanzania (TBS) Dkt Yusuph Ngenya na Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Viwango kutoka Zanzibar ,Hafsa Ali Slim.

Mkurugenzi Mkuu Shirika la viwango Tanzania (TBS) Dkt Yusuph Ngenya,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu tuzo za ubora za kitaifa kwa mwaka 2022-2023 leo Oktoba 27,2022 jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Viwango ambaye amemwakilisha Mkrugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS)Bi.Hafsa Ali Slim,akielezea jinsi walivyojipanga kutoa elimu kwa upande wa Zanzibar ili waweze kushiriki kwa wingi zaidi kuhusu tuzo za ubora za kitaifa kwa mwaka 2022-2023 leo Oktoba 27,2022 jijini Dodoma.

About the author

mzalendoeditor