Featured Kitaifa

RAIS SAMIA ASHUSHA NEEMA KWA WALIOONDOLEWA KWA VYETI FEKI

Written by mzalendoeditor

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof.Joyce Ndalichako,akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa tamko la Serikali kuhusiana na watumishi  14,516 waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi na waliondolewa kwenye utumishi wa umma leo Oktoba 26,2022 jijini Dodoma.

………………………

Na Alex Sonna-DODOMA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameridhia kurejesha michango ya watumishi 14,516 waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi na waliondolewa kwenye utumishi wa umma ambapo Sh.Bilioni 46.8 zitatumika  .

Hayo yamesemwa leo Oktoba 26,2022 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na watu wenye ulemavu, Prof.Joyce Ndalichako,wakati akitoa tamko la Serikali kuhusiana na watumishi hao amesema hatua hiyo ya serikali imetokana na ombi la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuangalia namna ya kuwafuta jasho watumishi hao.

Prof.Ndalichako amesema kuwa baada ya uchambuzi kufanyika Rais ameridhia kuwa watumishi wote walioondolewa kazini kwa kughushi vyeti warejeshewe michango yao tu waliyokatwa kwenye mishahara na kuwasilishwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.”

“Mifuko ya PSSSF na NSSF itarejesha michango ya wafanyakazi iliyowasilishwa kwenye mifuko hiyo bila kuhusisha michango ya mwajiri.Marejesho ya michango ya watumishi itaanza kufanyika Novemba mosi, mwaka huu, mtumishi husika atatakiwa kwenda kwa aliyekuwa mwajiri wake,”amesema Prof.Ndalichako

Aidha amefafanua kuwa mtumishi alikuwa akikatwa asilimia tano ya mshahara kuchangia mfuko wa PSSSF na kwa NSSF ni asilimia 10 bila kuhusisha malipo yeyote ya ziada.

“Kinachorejeshwa ni asilimia tano tu ambayo ilikatwa kwenye mshahara wa mtumishi na kuwasilishwa kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii, mifuko itafanya marejeshi ya ile asilimia tano, hayatahusisha michango iliyokuwa inawasilishwa na mwajiri,”amesema.

Prof.Ndalichako amewaelekeza watumishi hao wanatakiwa kwenda na picha mbili, nakala ya taarifa za kibenki kwenye akaunti iliyo hai na nakala ya kitambulisho cha taifa au mpiga kura au leseni ya udereva.

“Mtumishi atatakiwa kujaza hati ya ridhaa kwa aliyekuwa mwajiri wake, aidha waajiri watawajibika kuwasilisha kwenye mifuko hati za ridhaa pamoja na nyaraka nyingine zinazohusu ulipaji wa mafao kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya mifuko husika,”amesema

Hata hivyo ametoa wito kwa watumishi hao kuhakikisha wanakamilisha taratibu hizo ili kuwezesha mifuko kuwarejeshea michango yao.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Jenista Mhagama, ameawaagiza waajiri wote kuwajibika kwa kutoa ushirikiano kwa watumishi hao huku akitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufuatilia suala hilo.

“Waajiri wahakikishe waandaa madawati ya msaada ili kufanikisha kwa urahisi zoezi hilo,pia naagiza TAKUKURU kuanzia sasa wahakikishe wanatumia kila mbinu kuzuia kitendo au kiashiria cha rushwa, na watumishi nao wawe waaminifu,”amesema.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof.Joyce Ndalichako,akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa tamko la Serikali kuhusiana na watumishi  14,516 waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi na waliondolewa kwenye utumishi wa umma leo Oktoba 26,2022 jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Jenista Mhagama,wakati akitoa tamko la Serikali kuhusiana na watumishi  14,516 waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi na waliondolewa kwenye utumishi wa umma leo Oktoba 26,2022 jijini Dodoma.

About the author

mzalendoeditor