Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) Dkt. Michael Ng’umbi,,akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Oktoba 24,2022 jijini Dodoma.
………………………………
Na Alex Sonna-DODOMA
TAASISI ya Elimu ya Watu wazima (TEWW) imeeleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2021/2022 imehamasisha kurejea shuleni kwa wasichana 3,333 walioshindwa kuendelea na elimu ya sekondari kwa sababu mbalimbali.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 24,2022 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt.Michael Ng’umbi,wakati akitoa taarifa kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
”Baadhi ya sababu hizo ni pamoja na mazigira magumu, kupata ujauzito au ndoa za utotoni kwa wenye umri kati ya miaka 13 hadi 21 ikiwa ni sawa na asilimi 111 ya lengo lililowekwa kupitia vituo 131 vinavyo hudumiwa na walimu 803.”amesema Dkt.Ng’umbi
Amesema kuwa kazi zilizofanywa na taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022, waliandaa na kuendesha mafunzo katika kampasi zake tatu Dar es Salaam, Morogoro na Mwanza.
Ambapo Programu tatu za mafunzo zilitolewa kwa njia ya ujifunzaji wa kawaida na kwa njia ya ujifunzaji huria na masafa.
“Programu hizo ni Elimu ya Watu Wazima na Mafunzo Endelezi, Elimu ya Watu Wazima na Maendeleo ya Jamii, na Elimu Masafa kwa ngazi za Astashahada, Stashahada na Shahada”amesema Dkt.Ng’umbi
Aidha amesema kuwa jumla ya wanafunzi 8,093 ambapo wanawake 4,644 na wanaume 3,449 walipata mafunzo hayo.
Pia, ameeleza kuwa taasisi hiyo ilifanya usajili wa wanafunzi wapya ambapo jumla ya wanafunzi 3,426 walisajiliwa katika programu tatu za TEWW kwa mwaka wa masomo 2021/22.
Aidha, jumla ya walimu na wasimamizi wa elimu ya watu wazima 2,355, walihitimu masomo yao katika mwaka 2021/22.
Vilevile, amesema katika kipindi hicho taasisi hiyo iliandaa mtaala wa mafunzo ya walimu wa elimu ya watu wazima katika maeneo ya ufundi na teknolojia.
Aidha, mafunzo hayo yanatarajiwa kuanza kutolewa kwa ngazi ya astashahada na stashahada katika mwaka wa masomo 2023/24 baada ya kuidhinishwa na NACTVET.
“Kwa mwaka 2022/2023, TEWW inatarajia kuendelea na utekelezaji wa jukumu hili ikiwa ni pamoja na kukamilisha mtaala wa mafunzo ya walimu wa elimu ya watu wazima katika maeneo ya ufundi na teknolojia na kupata idhini ya NACTVET”amesema
Hata hivyo amesema kuwa katika mwaka 2021/2022, TEWW ilipokea jumla ya maombi 62 kutoka kwa wadau wakiomba usajili wa kuendesha vituo vya shule huria za sekondari Tanzania bara.
Ameeleza kuwa ni waombaji 58 waliokidhi vigezo na kusajiliwa kwa mwaka 2021/22.
Amesema kuwa katika mwaka 2022/2023, TEWW itaendelea kuboresha nyenzo za usimamizi wa utoaji wa elimu nje ya mfumo rasmi katika ngazi ya elimumsingi,ili kuhakikisha ubora wa mafunzo yanayotolewa na vituo vinavyosajiliwa.
Na kuongeza kuwa ” kwa 2022/2023, TEWW itaendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Tekonolojia katika kuandaa Juma la Elimu ya Watu Wazima kwa mwaka 2023. Vile vile, TEWW itahamasisha, kusajili na kufundisha wanafunzi 3,000 wa mradi wa SEQUIP kwa mwaka 2023,”Dkt.Ng’umbi
Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) Dkt. Michael Ng’umbi,,akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Oktoba 24,2022 jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) Dkt. Michael Ng’umbi,akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kutoa taarifa kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Oktoba 24,2022 jijini Dodoma.