Featured Kitaifa

WAZIRI BASHUNGWA AIPONGEZA KAMANDI YA NCHI KAVU UTEKELEZAJI MAJUKUMU YAKE

Written by mzalendoeditor

WAZIRI  wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimmiwa Innocent Lugha Bashungwa , ameipongeza Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu kwa juhudi na weledi katika utekelezaji wa majukumu yake. Ameyasema hayo alipofanya ziara yake ya kwanza ya kutembelea Makao Makuu ya Jeshi la Nchi Kavu yaliyopo eneo la Msangani – Kibaha mkoani pwani.
Akiwa Makao Makuu ya Kamandi, Mheshimiwa Bshungwa alipata fursa ya kupatiwa Taarifa Fupi ya Kamandi kuhusu majukumu ya Kamandi, muundo, eneo la uwajibikaji, hali ya Kamandi, mipango ya baadaye ya Kamandi, changamoto pamoja na mapendekezo.
Akiongea na Wanadhimu Wakuu wa Makao Makao Makuu ya Kamandi, Waziri Bashungwa amebainisha kuwa Jeshi bora linatokana na askari waliofunzwa vizuri, na wenye nidhamu. Mafunzo duni huzaa askari legelege na wasiojiamini. Jeshi letu lina sifa ya kutoa mafunzo bora na thabiti kwa askari wetu, hivyo kuwa na Jeshi lenye nidhamu, na linalojiamini katika utekelezaji wa majukumu yake.

Aidha, amewaasa kuwa macho wakati wote huku tukiendelea kuangalia na kuchukua hatua stahiki kwa viashiria vyovyote vinavyotishia amani na usalama wa Taifa letu. Tuitunze na kuilinda amani ya nchi yetu kama mboni ya jicho, kwani ikitetereka uzoefu unaonyesha ni vigumu sana kuirejesha.

Kuhusu Matishio ya amani, Waziri Bashungwa amekumbusha kuwa tunapaswa kufahamu kuwa, matishio ya amani na usalama yanaendelea kubadilika siku hadi siku. Kwa sasa, pamoja na kubadilisha kwa kiasi kikubwa, conventional warfare inachukua sehemu ndogo sana ya nadharia ya vita. Haya Matishio haya yanajumuisha ugaidi, matishio ya kimtandao (cyber security challenges), uhalifu ya baharini, matishio yanayotokana na mabadiliko ya tabia ya nchi, na majanga mbalimbali.

Matishio yote haya kwa pamoja yanaongeza umuhimu wa kufanya mafunzo zaidi, utafiti, na ubunifu unaokwenda sambamba na kasi ya ukuaji/mabadiliko ya kiteknolojia, ambapo mbinu, zana na vifaa nazo zinahitaji kubadilika kuendana na mahitaji ya wakati na aina ya matishio husika.

Wizara kwa upande wake inawahakikishia kufanya yale yaliyo ndani ya uwezo wake kuona Jeshi letu linatimiziwa mahitaji yake, ili nalo liweze kutekeleza majukumu yake. Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, inajali na kuthamini mchango mkubwa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika Ulinzi na Usalama wa nchi yetu.

Wakati wote Serikali hii imekuwa sikivu, na imekuwa ikizifanyia kazi changamoto mbalimbali zilizowasilishwa. Kwa kuwa ndiyo kwanza nimeanza majukumu tangu kuteuliwa, naomba mnipe muda kidogo kupitia changamoto mbalimbali ambazo nina imani mliishawasilisha kwa mtangulizi wangu, ili kuainisha zipi zimefanyiwa kazi na zipi bado ili nami nione pa kuanzia.

Alihitimisha Hotuba yake kwa kuwafikishia salamu za Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Mama Samia Suluhu Hassan, kuwa anatambuwa na kuthamini kazi kubwa na ya kizalendo inayoendelea kufanywa, na anatambua umuhimu wa Kamandi hii ya Jeshi la Nchi Kavu kwa Jeshi letu na taifa kwa ujumla.

Aidha, aliwahakikishia kuwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu anayo dhamira ya dhati ya kupunguza na hatimaye kuzimaliza changamoto zinazotukabili kama ilivyojidhihirisha kupitia jitihada mbalimbali zinazoendelea.

About the author

mzalendoeditor