Featured Kitaifa

KIPANGA AZITAKA HALMASHAURI KUTENGA BAJETI KUWEZESHA MAAFISA ELIMU YA WATU WAZIMA

Written by mzalendoeditor

 

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga akizungumza wakati wa kufunga Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima yaliyofanyika katika Viwanja vya DUCE Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga akipokea maelezo kutoka kwa mmoja washiriki katika maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima yaliyofanyika katika Viwanja vya DUCE Jijini Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga akipokea maelezo kutoka kwa mmoja washiriki katika maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima yaliyofanyika katika Viwanja vya DUCE Jijini Dar es Salaam.  Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga akipokea maelezo kutoka kwa mmoja washiriki katika maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima yaliyofanyika katika Viwanja vya DUCE Jijini Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga akizungumza wakati wa kufunga Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima yaliyofanyika katika Viwanja vya DUCE Jijini Dar es Salaam Kamishna wa Elimu, Dkt. Lyabwene Mtahabwa akizungumza wakati wa kufunga Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima yaliyofanyika katika Viwanja vya DUCE Jijini Dar es Salaam Amidi, Shule Kuu ya Elimu Dkt.Eugenia Kafanabo akizungumza wakati wa kufunga Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima yaliyofanyika katika Viwanja vya DUCE Jijini Dar es Salaam

………………………..

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga ametoa wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya kuwawezesha Maafisa wanaosimamia Elimu ya Watu Wazima kuwafikia walengwa kwa urahisi.

Mhe. Kipanga ametoa wito huo wakati akifunga maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima yaliyofanyika katika Viwanja vya DUCE Jijini Dar es Salaam ambapo amesema kwa kufanya hivyo itawezesha utekelezaji wa shughuli za elimu ya watu wazima katika eneo husika kwa ufanisi.

Amesema katika kuipa uhai elimu ya watu wazima pamoja na kutengewa bajeti maafisa elimu wanaoshughulika na eneo hilo ndani ya Mikoa na Halmashauri wanapaswa kuhakikisha wanahamasisha, kuanzisha, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa Programu mbalimbali za Elimu ya Watu Wazima.

“Niwasihi Maafisa Elimu Elimu ya Watu Wazima pamoja na kusimamia kazi katika maeneo yenu shirikianeni na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kuendeleza jitihada za kuhakikisha kuwa madarasa ya MEMKWA yanasimamiwa na kuwa na vitendea kazi vinavyokidhi mahitaji ya ufundishaji na ujifunzaji,” amesema Mhe Kipanga.

Akizungumzia mapitio ya Sera na mitaala yanayoendelea Mhe. Kipanga amesema Wizara bado inapokea maoni ya wadau kuhusu maboresho hayo huku ikiendelea na uchambuzi wa maoni ambayo yamepokelewa ili kukamilisha kazi hiyo.

Amesema kumekuwa na taarifa ambazo si za kweli zinazosambaa kwenye mitandao zikisema kuwa “Sera ya Elimu inayotarajiwa kuzinduliwa hapo baadae elimu ya msingi itakomea darasa la sita.”

“Nilikuwa kwenye Kongamano la Wanataaluma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakati nazungumza nilisema kuwa tunaendelea na mapitio ya Sera ya Elimu na kwamba kuna maoni mbalimbali yameshatolewa na katika uchambuzi yapo maoni yaliyosema elimu ya msingi ikomee darasa la sita na baada kumaliza kuwe na mifumo na njia mbili kuu ambazo zinawapeleka vijana kwenye taaluma na ujuzi. Sasa zipo nukuu kwenye mitandao zikisema nimesema elimu ya msingi mwisho darasa la sita, si kweli,” amefafanua Mhe. Kipanga.

Aidha amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata fursa ya kupata elimu iliyo bora na ndio maana imeweka Sera ya Elimu bure kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita huku ikiwarudisha shule wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali waweze kuendela na masomo ili watimize ndoto zao.

Akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara katika kilele hicho Kamishna wa Elimu, Dkt. Lyabwene Mtahabwa amesema katika kukabiliana na changamoto ya idadi ya watu wasiojua Kusoma, Kuandika na Kuhesabu, Wizara inatekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kisomo cha Elimu kwa Umma ambao unalenga kuboresha programu za kisomo na elimu kwa njia mbadala. Pia imeandaa “National Qualification Framework” mfumo ambao kwa mara ya kwanza umetambua programu za Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi.

Maonesho ya Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima yaliyofanyika Jijini Dar es Salam kuanzia Oktoba 17-21, 2022 yalikuwa na kaulimbiu isemayo “Kuboresha mazingira ya kujifunza kusoma na kuandika yatakayozingatia ubora, usawa na ujumuishi wa makundi yote” na yameshirikisha Vyuo Vikuu, Taasisi zilizo chini ya Wizara, Maafisa Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi Wilaya na Mikoa yote Tanzania Bara, Mashirika ya Kimataifa pamoja na wadau mbalimbali wanaojishughulisha na utoaji wa Elimu ya Watu wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi hapa nchini.

About the author

mzalendoeditor