Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia Wananchi wa Mkoa wa Geita kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Kalangalala mkoani humo.
………………
OR -TAMISEMI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za ujenzi wa ofisi za wafanyabiashara wadogo (machinga) kwa kila Mkoa Sh.Milioni 10 huku akiagiza Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuandaa ramani maalum ya majengo hayo kulingana na fedha iliyotolewa.
Ameyasema hayo leo Oktoba, 15, 2022 wakati akiwahutubia wananchi wa Mkoa wa Geita katika ziara yake ya kikazi ya siku moja.
Amesema tayari fedha hiyo ipo TAMISEMI hivyo wahakikisha wanakamilisha zoezi hilo la kuandaa ramani kwa wakati na ujenzi wake uanze.
Amewaagiza Wakuu wa Mikoa yote nchini kuhakikisha wanatenga maeneo ambayo machinga watapewa bure kwa ajili ya kujenga ofisi hizo.
“Wakuu wa Mikoa chagueni maeneo ya karibu na si maeneo ya
uchochoroni, “amesema Mhe.Rais.