Featured Kitaifa

WAZIRI CHANA:’TUTAENDELEA KUSHIRIKIANA NA HISPANIA’

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Maliasilia na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Taifa la Hispania iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

…………………………

Waziri wa Maliasilia na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana ameihakikishia Serikali ya Ufalme wa Hispania kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na nchi hiyo katika kukuza na kuimarisha uhusiano uliopo kwa manufaa ya nchi na watu wake.

Mhe. Dkt. Pindi Chana ametoa kauli hiyo katika hafla ya maadhimisho Siku ya Uhuru wa Taifa la Hispania iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kushirikiana  kwa karibu na Serikali ya Ufalme wa Hispania katika kukuza na kuimarisha uhusiano wetu kwa maslahi mapana ya nchi zetu na wananchi,” alisema Mhe. Dkt. Pindi Chana.

Ameishukuru Hispania kwa kuendelea kuisaidia Tanzania kupitia sekta za maji, afya, umeme vijijini na kilimo na kuongeza kuwa ni matumaini yake kwamba ushirikiano huo utakuwa na kufikia sekta nyingine nyingi za kiuchumi.

Mhe. Dkt. Pindi Chana pia ameishukuru Hispania kwa kuijumuisha Tanzania kuwa moja ya nchi za Afrika zitakazonufaika na Sera Maalum ya Nchi za Afrika iliyoanzishwa mwaka 2019.

Amesema Hispania imekuwa mstari wa mbele katika maeneo ya afya, lishe, elimu, mabadiliko ya tabia nchi na usawa wa kijinsia, maeneo ambayo ni ya kipaumbele pia kwa Tanzania na kuongeza kuwa ni matumaini yake kwamba Tanzania na Hispania zitaendelea kushirikiana katika maeneo hayo kwa maslahi mapana ya nchi hizo.

“Kwa miaka mingi Serikali ya Hispania imekuwa mstari wa mbele katika maeneo ya afya, lishe, elimu, mabadiliko ya tabia nchi na usawa wa kijinsia, hay ani maeneo ambayo Tanzania ni kipaumbele chake pia nina uhakika kuwa Tanzania na Hispania zitaendelea kushirikiana katika maeneo hayo kwa maslahi mapana ya nchi zetu” alisema.

Akiongelea kuhusu uhusiano wa kibiashara Dkt. Pindi Chana ametoa wito wa kuongezwa kwa biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo na kuongeza kuwa ujazo wa biashara kati ya nchi hizo kwa mwaka 2021 ulikuwa sawa na Shilingi Bilioni 183.3.

Akiongelea Utalii Dkt. Pindi Chana alisema watalii kutoka Hispania wamekuwa wakiitembelea Tanzania lakini watalii hao walipungua kutokana na janga la ugonjwa wa COVID 19 kutoka watalii 18,838 kwa mwaka 2019 hadi watalii 13,150 kwa mwaka  2021.

Alitoa wito kwa watalii wa Hispania kuja kwa wingi kuitembeleea Tanzania kutokana na kuwa na vivutio vya kipekee  duniani na hawatasahau ujio wao hapa nchini.
Awali akimkaribisha Dkt. Chana katika hafla hiyo Balozi Mteule wa Ufalme wa Hispania nchini Mhe. Jorge Moragas Sánchez alisema Serikali yao ina nia ya kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa kuingiza maeneo mengi zaidi ya ushirikiano na kufanya kazi pamoja na kuiletea nchi maendeleo.

Alitaja mpango mradi wa upanuzi wa Mto Msimbazi jijini Dar es Salaam ambao watakaoshirikiana na Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania kama mfano mmojawapo

“Tumekuwa na ushirikiano mzuri kati ya nchi zetu, tunataka kushirikiana zaidi katika maeneo ya Maendeleo, mfano ni kupitia mradi wa upanuzi wa Mto Msimbazi jijini Dar es Salaam ambako tunashirikiana na Benki ya Dunia na Serikali kufanya kazi hiyo,” alisema.

Waziri wa Maliasilia na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Taifa la Hispania iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Maliasilia na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akiwa na Balozi Mteule wa Ufalme wa Hispania nchini Mhe. Jorge Moragas Sánchez wakiimba wimbo wa Taifa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Taifa la Hispania iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Maliasilia na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akiwa na Balozi Mteule wa Ufalme wa Hispania nchini Mhe. Jorge Moragas Sánchez wakiimba wimbo wa Taifa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Taifa la Hispania iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya washiriki wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Taifa la Hispania iliyofanyika jijini Dar es Salaam wakijumuika.

About the author

mzalendoeditor