Featured Kitaifa

WAZIRI PINDI CHANA AZINDUA BODI YA WAKURUGENZI TAWA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana leo tarehe 12 Oktoba, 2022 amezindua Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA aliyoiteua hivi Karibuni.

Akizungumza katika hafla ya Uzinduzi iliyofanyika Makao Makuu ya TAWA Mkoani Morogoro, Dkt. Chana amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kwa kumteua Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA na kuwapongeza wajumbe Wote wa Bodi hiyo kuteuliwa kuiongoza TAWA.

“Nichukue nafasi hii Kumshukuru sana Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan Kwa kumteua “Chairman” (Mwenyekiti) wetu Mej. Jen.(Mstaafu) Hamis Semfuko asante sana ametuletea “Chairman” hodari kabisa na Kwakweli tuna matumaini makubwa sana na wewe” amesema

“Kwa dhati kabisa nawapongeza Wakurugenzi wa Bodi wote Kwa kuteuliwa kuiongoza Bodi hii ya TAWA” ameongeza.

Dkt. Pindi Chana amesema uteuzi wa bodi hiyo umefanyika Kwa umakini mkubwa na kuzingatia weledi na uzoefu wa wakurugenzi hao ambao utaisaidia taasisi hiyo kufikia malengo hususani katika utekelezaji wa mikakati ya kuzuia ujangili, kuongeza idadi ya watalii na mapato na hivyo kuendeleza sekta ya Wanyamapori.

Aidha Waziri Pindi Chana ametoa rai Kwa bodi hiyo Kuweka mikakati ya Changamoto ya ongezeko la matukio ya Wanyamapori wakali na Waharibifu na uvamizi wa mifugo hifadhini.

Sambamba na hilo, Mhe. Dkt. Chana amewataka watu wenye tabia ya kuingiza mifugo ndani ya hifadhi kuacha vitendo hivyo mara moja.

“Nitumie nafasi hii kuushirikisha Umma kwamba maeneo ya hifadhi zetu siyo maeneo ya kulishia mifugo, haya ni maeneo ambayo tunapaswa kuyalinda Kwa maslahi ya Wote” amesema

Dkt. Chana ameongeza vitendo vya kuingiza mifugo hifadhini vinaleta athari kubwa Kwa kukausha vyanzo vya maji, kuharibu mazingira na athari zake kuwa kubwa Kwa Taifa, hivyo amewaomba wananchi washirikiane na Serikali katika kuhifadhi maeneo yaliyohifadhiwa Kwa lengo la uhifadhi Kwa maslahi ya Nchi yetu.

Mbali na shughuli ya Uzinduzi wa Bodi, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana alizindua mitambo mbalimbali iliyonunuliwa na TAWA Kwa fedha za UVIKO – 19 ambayo ni mashine za kuchima visima vya maji, matreka, “caterpillars”, boti maalumu kwa ajili ya doria n.k

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Elaimani Sedoyeka amesema TAWA ina maeneo makubwa takribani asilimia 10 ya maeneo yote Nchini, hivyo anatumaini kwamba itabuni mikakati mbalimbali ya kuongeza idadi ya watalii, mapato na kuimarisha shughuli za Uhifadhi, kuboresha miundombinu ya Utalii, kujenga uwezo wa watumishi pamoja na matumizi ya teknolojia katika kuongeza ufanisi na tija kiutendaji.

Akielezea mikakati ya Bodi mpya ya TAWA, Mwenyekiti wa Bodi Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis Semfuko amesema mkakati wa kwanza ambao Bodi itaupa kipaumbele ni kupunguza migongano kati ya watu na Wanyamapori “Human Wildlife Conflicts” Ili kuhakikisha TAWA inakuwa chombo ambacho kinakuwa na faida Kwa Serikali na Umma.

Kamishna wa Uhifadhi TAWA ambaye pia ni Katibu wa Bodi iliyozinduliwa leo, Mabula Misungwi Nyanda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Kwa kumteua Mej. Jen. Mstaafu Hamis Semfuko kwa awamu nyingine Ili aendelee kufanikisha kazi kubwa aliyokwisha ianzisha.

Aidha amempongeza Mwenyekiti huyo Kwa kuendelea kuaminiwa na kuteuliwa kuiongoza TAWA na kumuahidi ushirikiano Wakati Wote wa utekelezaji wa majukumu ya Bodi Ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

       

About the author

mzalendoeditor