Featured Kitaifa

SERIKALI YAZINDUA KITUO CHA OPARESHENI YA MATUKIO YA MLIPUKO NA DHARURA.

Written by mzalendoeditor

 
Na Englibert Kayombo – WAF Dodoma.
 
Serikali kupitia Wizara ya Afya imefungua Kituo maalum cha oparesheni ya matukio ya mlipuko na dharura kwa ugonjwa wa Polio Jijini Dodoma.
 
Kituo hicho kimefunguliwa leo na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi kitaiwezesha Serikali kuchukua hatua za awali katika kukabiliana na matukio ya dharura na ufuatiliaji wa karibu wa magonjwa ya mlipuko.
 
“Hivi karibuni matukio ya dharura yamekuwa yakitokea duniani kote kama vile milipuko ya magonjwa ya Polio, Kipindupindu, UVIKO – 19, Ebola na Homa ya Mgunda, vituo hivi vinawezesha uratibu wa shughuli mbalimbali katika kuchukua hatua za pamoja za kukabiliana na matukio haya” amesema Prof. Makubi.

Amesema kuwa kituo hicho kitakuwa mahususi kwa ajili kufanya uratibu na ufuatiliaji wa matukio ya dharura na mlipuko pamoja na kutoa maelekezo kwenda sehemu nyingine kwa ajili ya utekelezaji wa hatua mbalimbali za kukabiliana na matukio hayo.

Amesema kuwa kwa sasa Serikali kwa kushirikiana na Wadau imeweza kuanzisha kituo hicho kwa ngazi ya Taifa ikiwemo sehemu ya kituo kikuu cha uratibu wa matukio ya dharura ya afya kisekta huku juhudi nyinginezo zikiendelea kuanzisha vituo vingine katika ngazi ya Kanda na Mikoa.

“Hatuwezi kuwa na kituo hiki ngazi ya Taifa pekee, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alipokuwa katika shughuli za ufuatiliaji na udhibiti wa ugonjwa wa Ebola usiingie nchini akiwa Kagera aliahidi kwamba tunakwenda kujenga vituo vingine kwa ajili ya kukabiliana na majanga, vituo hivyo ni pamoja na vituo vya oparesheni ya matukio ya mlipuko na dharura” amesema Prof. Makubi.

Aidha Prof. Makubi amewataka Wadau wa Sekta ya Afya kushirikiana na Serikali katika kujenga vituo hivyo katika ngazi ya Kanda na Mikoa huku akitilia mkazo zaidi katika uanzishwaji wa vituo hivyo katika Mikoa ilipoyo pembezoni au mipakani.

Prof Makubi amelishukuru Shirika la Bill and Melinda Gates Foundation; Shirika la Afya Duniani (WHO) eHealth, CDC pamoja na wadau wengine kwakufanikisha kukamilika kwa kituo hicho kilichogharimu kiasi cha Shilingi Milioni 176 ikiwemo pamoja na ununuzi wa vifaa na thamani za ofisi.

Akizungumiza taarifa ya uchanjaji wa chanjo ya Polio, Prof. Makubi amesema awamu ya kwaza ilifanikisha kuchanja Watoto 1,130,261wenye umri wa chini ya miaka 5 sawa na asilimia 115.8; Awamu ya Pili Watoto 12,131,049 sawa na asilimia 117.8; Awamu ya tatu Watoto 14,690,597 sawa na asilimia 118.6.

“Sambamba na juhudi zinazoendelea kwa sasa katika kuzuia mlipuko wa Polio, Tanzania imeweza kuzuia uingizwaji wa virusi pori vya ugonjwa wa Polio. Hii iliwezesha nchi kupata sifa ya kutangazwa kuwa nchi huru dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Polio (Polio free country) tangu mwaka 2015” amesema Prof. Makubi.

Ametoa rai kwa viongozi na watumishi wote wa afya kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili a sifa tuliyopata Tanzania isije kupotea huku akiitaka Mikoa na Wilaya chache ambazo hazifanyi vizuri katika uchanjaji viongozi wasimame vizuri ili malengo ya uchanjaji yafikiwe.
 

About the author

mzalendoeditor