Featured Kitaifa

WAZIRI MKENDA ARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA VETA MKOANI GEITA

Written by mzalendoeditor

Na Mathias Canal, WEST-Geita

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda amepongeza kasi ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi stadi-VETA katika mkoa wa Geita.

Ametoa pongezi hizo leo tarehe 10 Octoba 2022 wakati akizungumza na uongozi wa VETA mara baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa VETA akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Geita.

Pamoja na pongezi hizo Waziri Mkenda ametaka usimamizi madhubuti wa ujenzi wa vyuo hivyo ikiwa ni pamoja na kusimamia ubora wa stadi na ufundi zitolewazo katika vyuo hivyo.

Waziri MKenda amesema kuwa kazi ya usimamizi wa ujenzi kimepewa chuo cha ufundi Arusha hivyo wanapaswa kusimamia kazi iende vizuri na kukamilisha ujenzi haraka.

β€œMkifanya vizuri tutawasifu, sisi sio kazi yetu kuwaponda ila tunataka kazi iende na kwa hapa Geita hongereni mnaendelea vizuri na chuo cha ufundi Arusha nataka nione wanabadilika na kama wasipobadilika tutawabadilisha” Amekaririwa Waziri Mkenda na kuongeza kuwa

β€œNawapongeza kwa kubaini changamoto za ujenzi na hatimaye kurekebisha kadhia hizo, na nimeagiza Menejimenti, Wahandisi na wataalamu kutoka chuo cha Ufundi Arusha ambao ndio wasimamizi wa mradi huu waweze kwenda Simiyu na Geita kukagua ujenzi wa VETA”

Waziri Mkenda amesema kuwa kazi hizo walizopewa chuo cha ufundi Arusha ni kipimo chao hivyo wanapaswa kusimamia kwa uadilifu na umakini mkubwa na endapo wasiposimamia ipasavyo Wizara itachukua hatua abazo ni kubwa.

Kuhusu mpango wa kujenga kampasi au chuo kikuu cha madini, Waziri Mkenda amesema kuwa Wizara yake inaunga mkono mawazo hayo na kwa kuwa kanda ya ziwa ni kitovu katika sekta ya madini hivyo haitakuwa vibaya chuo hicho kujengwa kanda ya ziwa.

About the author

mzalendoeditor