Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Mhashamu Beatus Michael Kinyaiya OFM Cap,akipanda mti wa kumbukumbu katika bustani iliyopo ndani ya Shule ya Sekondari ya Mt.Chistopher iliyopo Parokia ya Kibaigwa,kama sehemu ya uzinduzi rasmi wa shule hiyo.(Picha na Ndahani Lugunya)
………………………
Na Ndahani Lugunya,Kongwa
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma la Dodoma Mhashamu Beatus Michael Kinyaiya OFM Cap,amefungua rasmi Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Christopher iliyopo Parokia ya Kibaigwa Dekania ya Kongwa,na kutoa Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 10 wa Shule hiyo.
Akizungumza katika ufunguzi huo Askofu Kinyaiya alisema kwamba, pamoja na mambo mengine dhumuni na lengo la Kanisa Katoliki kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kuanzisha shule mbalimbali za msingi na Sekondari ,ni kuwalea watoto katika maadili mema na tabia njema kwa manufaa yao wenyewe,familia na Taifa kwa Ujumla.
Aliwaomba wazazi na walezi kuendeleza malezi na makuzi ya kimaadili na tabia njema kwa Vijana wao pindi wanapohitimu masomo yao katika Shule za Kanisa,na kamwe wasiwe chanzo cha kuharibu maisha ya watoto yanayotengenezwa vema pindi wawapo Shuleni.
Hata hivyo Askofu Kinyaiya aliwataka wanafunzi wanaosoma shuleni hapo kuishi kwa malengo pindi wawapo shuleni hapo,na wawe na watu wa kuwatazama kama mfano mwema wa kuigwa katika kutimiza ndoto zao.
“Na ninyi vijana naomba katika maisha yenu muwe na watu wa kuwaiga kama mfano kwenu.usiishi bila kuwa na vision (maono) usiishi bila kuwa na picha mbele yako unayolenga kutakuwa kuwa kama hiyo picha.na ni lazima upande usiku mchana ili uweze kufikia hicho ambacho umekipenda mbele ya macho yako,” alisema Askofu Kinyaiya
Aidha aliwataka wanafunzi hao kutambua kwamba chochote wanachofanya katika maisha ni kwa ajili ya manufaa yao wenyewe,hivyo kila kitu wanapaswa kukifanya kwa uwezo wao wote,iwe katika kusoma au kazi mbalimbali za maisha ya kila siku.
Katika hatua nyingine Askofu Kinyaiya aliwataka vijana watakaohitimu Kidato cha Nne Mwezi Novemba kwenda kuwa mabalozi wa utunzaji mazingira.
Awali akisoma Risala Mkuu wa Shule Mwl Bernard Kopoka alisema kwamba,Shule ya Sekondari ya Mt.Christopher ilianzishwa rasmi mwaka 2005 ikiwa chini ya umiliki wa mtu binafsi,ambapo mwaka 2020 mwezi Julai Shule ilibadili umiliki wake na kuwa chini ya Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.
“Mpaka sasa Shule yetu ya Mt.Christopher ina jumla ya Walimu 10 wapishi wawili walinzi wawili Patron kwa ajili ya Wanafunzi wa kiume mmoja,Matron kwa ajili ya wanafunzi wa kike mmoja na Wanafunzi 150 ikiwa ni mikondo ya Sayansi na Sanaa.
Aidha Shule ikiwa chini ya umiliki wa Jimbo tumuweza kutatua changamoto zifuatazo,kwanza kabisa ni uboreshaji wa miundombinu hasa maabala,jiko jipya la kisasa pamoja na kuweza kuwatoa wanafunzi wetu waliokuwa wanaishi mitaani na sasa wanaishi katika Mabweni yetu hapa Shuleni.
Pia tumeweza kuongeza vifaa vya Maabara ili kuweza kukidhi mahitaji ya Wanafunzi wetu hasa kwa somo la Sayansi,ambapo sambamba na hilo tumeweza kukabiliana na changamoto ya upungufu wa vyoo pamoja na majengo kuwa na viwango vinavyokidhi ufundishaji na kujisomea,” alisema Mwl.Kopoka.
Kwa upande wake Meneja wa Shule ya Sekondari ya Mt. Christopher ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Mt.Theresia wa Mtoto Yesu-Mlali Padri Emmanuel Ndechihilo,alimshukuru Askofu Mkuu Kinyaiya kwa kutekeleza vema dira ya Elimu katika Jimbo lake.
“Shule za Sekondari zipo nyingi lakini sisi tunataka tuweje,tutaionaje Christopher ya miaka mitano kumi ishirini hamsini ijayo?.kwanza kabisa Baba Askofu napenda kukuhakikishia kwamba nashika yale ambayo Shule zote zinashika yaani nidhamu na ufaulu.
Lapili tunataka tuweke kitu cha Human Development (Maendeleo ya Binadamu) mtu alelewe katika kukua kwake na kuendeleza uwezo wake na vipaji vyake alivyo navyo.tutaanza na programs (Mipango) ambazo ndani yake vifaa vyake vipo ambazo hazihitaji mtu afanyie mtihani. Tuwe na watu wa kutengeneza kompyuta program bila kufanyia mtihani cha msingi kama unayo hiyo interest (shauku) uende huko,tuwe na ushonaji si kwa ajili ya kufanyia mtihani bali anaetaka aende kujifunza ushonaji,tuwe na program ya ufundi bomba si kwa ajili ya kufanyia mtihani ili pia anaetaka aende huko tuwe na mafundi umeme na vitu kama hivyo,” alisema Padri Ndechihilo.
Akitoa neno la Shukrani kwa niaba ya Wazazi wote Ndugu Noel Kirway aliwataka wanafunzi wote wanaosoma Shuleni hapo kusoma kwa bidii na kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika kila jambo wanalolifanya katika elimu yao.
Shule ya Sekondari ya Mt.Chistopher iliyopo Parokia ya Kibaigwa,ni miongoni mwa Shule 4 za Sekondari zilizopo katika Dekania ya Mt.Fransisko wa Asizi-Kongwa,zikiwa chini ya umiliki wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma,ambapo nyingine ni Shule ya Sekondari ya Mt.Padri Pio-Kibaigwa,Shule ya Sekondari ya Mt.Francisco-Kongwa pamoja na Shule ya Sekondari ya Mt.Crala-Mlali.