Waziri wa Madini, Dk. Dotto Biteko ( wa pili kulia) akipatiwa maelezo kuhusu mradi wa kinu cha kupoza umeme kutoka kwa Meneja anayehusika na miundombinu kutoka GGML, Eliakimu Kagimbo. Dk. Biteko alitembelea mgodi wa GGML pamoja na mradi huo unaojengwa na kampuni hiyo ili kupokea umeme wa Tanesco na kuuwezesha mgodi kuanza kutumia umeme wa Gridi ya Taifa badala ya umeme unaozalishwa kwa mafuta ya dizeli.
………………………..
NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Madini Dkt. Dotto Biteko ameeleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa kinu cha kupoza umeme (substation) kinachojengwa na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) ili kuwezesha mgodi huo kuachana na uzalishaji wa umeme wa mafuta na kuhamia kwenye umeme wa Gridi ya Taifa ambao ni nafuu zaidi.
Mgodi huo wa GGML unajenga kinu hicho kitakachokuwa na uwezo wa kupitisha umeme wenye kilovolt 13 kwenye mitambo yake ambapo hadi kikamilike kinatarajiwa kugharimu kiasi cha Sh bilioni 50.
Aidha, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) nalo linajenga njia ya kupeleka umeme katika mgodi wa GGML yenye urefu wa kilomita sita.
Hayo yamebainishwa katika ziara ya Waziri wa Madini aliyoifanya juzi katika Mgodi wa GGML uliopo Geita ambapo pamoja na mambo mengine alisema anaamini hadi kufikia Machi mwaka 2023, GGML itaanza kutumia umeme wa gridi ya Taifa.
“GGML wanataka kuhama kutoka kwenye matumizi ya umeme unaozalishwa kwa mafuta kwenda kwenye umeme wa TANESCO, kupitia substation inayojengwa kwa dola za Kimarekani milioni 20, na wamekwenda kwenye hatua nzuri, naamini mpaka itakapofika Machi mwaka kesho tutawasha umeme wa TANESCO kuendesha mgodi wetu hapa ndani,” amesema Dkt. Biteko.
Awali, Makamu Rais wa kampuni ya AngloGold Ashanti inayomiliki Geita Gold Mining Limited (GGML), Simon Shayo amesema kukamilika kwa mradi huo kutapunguza gharama za uendeshaji wa mgodi na uzalishaji wa umeme kwa asilimia zaidi ya 50.
Alisema mgodi wa GGML unatumia zaidi ya MW 40 zinazozalishwa kwa kutumia jenereta zinazotumia mafuta ya dizeli tangu mwaka 2018.
“Sasa tupo kwenye mchakato wa kujenga kinu cha kupoozea umeme chenye thamani ya karibu Shilingi za Kitanzania bilioni 50 na TANESCO watajenga njia ya kilomita sita kufikia hapa.
“Kwa hiyo hadi kufikia Machi mwaka 2023, tutakuwa tumeingia kwenye umeme wa TANESCO, na tutakuwa tumepunguza gharama yetu ya umeme kufikia asilimia 50, kutoka uniti moja kwa senti 19 kwenda kwenye unit moja kwa senti tisa (US $),” alisema.
Aidha, ilielezwa kuwa kukamilika kwa mradi huo wa kupeleka umeme kwenye Kampuni ya GGML kunatarajiwa kutaliwezesha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupata shilingi bilioni tano za kitanzania kwa mwezi zitakazotokana na mauzo ya umeme.