Na Innocent Mungy, Bucharest
Tanzania imechaguliwa miongoni mwa nchi 48 kati ya nchi 193 wanachama wa ITU kuwa katika Baraza la Shirika la Mawasiliano duniani – International Telecommunication Union (ITU) kwa mwaka 2023 hadi 2026. Tanzania ni miongoni mwa nchi 13 zinazowakilisha Bara la Afrika.
Baraza la ITU ni chombo cha Shirika la Mawasiliano Duniani chenye mamlaka ya kusimamia masuala ya kisera ya mawasiliano ya simu ili kuhakikisha kuwa shughuli za ITU, sera na mikakati inasimamiwa kikamilifu kwa kuzingatia mazingira ya mawasiliano leo yanayobadilika kwa kasi.
Mheshimiwa Nape Nnauye (Mbunge), Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Tanzania amethibitisha dhamira ya Tanzania katika ITU kwa miaka 4 itakayokuwa katika Baraza hilo.
“Napenda kusisitiza kuwa Tanzania imedhamiria kushirikiana na nchi nyingine wanachama, Sekretarieti ya ITU na ofisi za Kanda ili kuifanya ITU kuwa chombo muhimu cha kimataifa ambacho kina mchango mkubwa katika kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya nchi zote wanachama kama mjumbe wa Baraza la ITU” alisema Mhe.Nnauye.
Baada ya kumchagua Doreen Bogdan-Martin (Marekani) kuwa Katibu Mkuu wa ITU, na Tomas Lamanauskas (Lithuania) Naibu Katibu Mkuu na Wakurugenzi 3 wanaosimamia maeneo matatu ya msingi ya kazi za ITU, nchi wanachama wa Shirika hilo la ITU wamekamilisha uchaguzi wa Baraza Kuu la ITU na Bodi ya Kanuni za Redio.
Mario Maniewicz (Uruguay) alichaguliwa kuhudumu kwa muhula wa pili kama Mkurugenzi wa Sekta ya Mawasiliano ya Redio ya ITU, ambayo ina jukumu la kudumisha na kutekeleza mkataba wa Kanuni za Redio unaowianisha matumizi ya wigo wa kimataifa na mizunguko ya satelaiti, na kwa kuendeleza viwango vya kiufundi vinavyohusiana.
Seizo Onoe (Japan) amechaguliwa kuongoza Sekta ya Viwango vya Mawasiliano ya ITU, ambayo ina uanachama wa serikali, mashirika, na wataalam wa kiufundi kutoka duniani kote na inasimamia kuunda na kusimamia viwango vya kiufundi vya kimataifa vya mawasiliano ya simu na TEHAMA.
Dkt. Cosmas Zavazava (Zimbabwe) amechaguliwa kuwa Mkurugenzi mpya wa Sekta ya Maendeleo ya Mawasiliano ya ITU, ambayo inasimamia kuratibu juhudi za kimataifa za kuunganisha wasiounganishwa kupitia kuhamasisha maendeleo ya kidijitali yenye usawa na jumuishi, kuimarisha uwezo na miundombinu ya mataifa yanayoendelea, na kuzindua mipango ya kufanya teknolojia iweze kupatikana kwa kila mtu.
Wajumbe 12 walichaguliwa kuwa wajumbe wa Bodi ya Kanuni za Redio ITU. Ofisi hiyo inasimamia kudumisha na kutekeleza mkataba wa Kanuni za Redio, ambao unaunganisha matumizi ya wigo wa kimataifa na mizunguko ya satelaiti, pamoja na kuunda viwango muhimu vya kiufundi.
Kuanzia Januari 1, 2023, viongozi watano waliochaguliwa pamoja na Wajumbe 48 wa Baraza la ITU wataanza uongozi wa miaka minne hadi 2026.