Featured Kitaifa

RAIS SAMIA ARIDHIA SH.BILIONI 160 KUJENGA VYUMBA VYA MADARASA 8,000

Written by mzalendoeditor

WAZIRI  wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa,akizngumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Septemba 28,2022 jijini Dodoma kuhusu maandalizi ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza Januari, 2023.

………………………………….

Na Alex Sonna-DODOMA

RAIS  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameidhinisha  kutolewa kiasi cha shilingi Bilioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa mapya 8000  ya shule za sekondari  kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023 ambao ni zao la Elimumsingi bila ada.

Hayo yamesemwa leo Septemba 28, 2022 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa  akizngumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza Januari, 2023

Bashungwa amesema kuwa kwa mwaka 2023 takribani wanafunzi 1,148,512 wanatarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza ambapo ni wale walioanza darasa la kwanza mwaka 2016, ambapo serikali ilianza utekelezaji sera ya Elimu msingi bila ada Disemba mwaka 2015.

 ”Fedha hizo tayari zimeshaingia kwenye akaunti za shule za sekondari 2,439 zilizoainishwa kuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa kwa ajili ya kidato cha kwanza 2023.”amesema Waziri Bashungwa

Amesema kwa sasa fedha hizo zimeshatumwa na kupokelewa kwenye halmashauri zote 184, kulingana na upungufu uliowasilishwa na kila Halmashauri husika.

Idadi ya wanafunzi waliochanguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022 ilikuwa ni 907,802 ikilinganishwa na wanafunzi 422,403 waliohitimu kidato cha nne, hivyo kuhitaji kuongezeka miundombinu ya madarasa na vyoo yenye kutosheleza wanafunzi 485,399 wa ziada.
Ili kutatua changamoto hiyo, Serikali ya awamu ya sita ilitoa kiasi cha sh. Bilioni 240 zilizofanikisha ujenzi wa madarasa 12,000, shule shikizi 3,000 na mabweni 60.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi, idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza ilikuwa kubwa sana, kwa kulinganisha na miaka iliyotangulia.

Kwa mukatadha huo wanafunzi waliopo darasa la saba mwaka 2022, ndio zao la kwanza la matokeo ya Elimumsingi bila ada,”amesema Bashungwa.

Ameeleza kuwa katika hali ya kawaida matarajio ni kuwa nafasi zilizopo kwa ajili ya wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza, zitokane na uwepo wa shule mpya za sekondari, ujenzi wa miundombinu mipya na nafasi zilizoachwa na wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne.

“Hata hivyo, kwa mwaka 2023 wanafunzi wnaaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza wamekuwa ni wengi zaidi ukilinganisha na wanafunzi 454,902 wanaohitimu kidato cha nne 2022,”alisema Waziri Bashungwa.

Amefafanua kuwa kutokana na ongezeko la wanafunzi wanatarajia kujiunga na kidato cha kwanza kuwa kubwa mwaka 2023 ukilinganisha na nafasi 454,902 zitakazoachwa wazi na wanafunzi wa kidato cha nne.

Bashungwa amesisitiza kuwa pamoja na fedha za ujenzi wa madarasa mapya 8,000, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/22 ilitoa sh. Bilioni 108 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za kata 231.

Aidha, shule hizo ziko katika hatua mbalimbali za ukamilishaji na zikikamilika zinatarajia kupokea waafunzi Januari 2022.

Waziri Bashungwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanazisimamia halmashauri zao kuhakikisha madarasa hayo 8000 yanamalizika nadani ya miezi miwili kabla wanafunzi wa kidato cha kwanza kuanza masomo.

Katika hatua nyingine Waziri Bashungwa amemuagiza Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia elimu DKT. Charles Msonde kufuatilia kwa kina suala la ajira mpya za walimu kwani kunamalalamiko mengi ya walimu wa ajira mpya kutolipya stahiki zao.

About the author

mzalendoeditor