Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizindua Jengo la Wodi ya Wagonjwa wa Saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando Jijini Mwanza leo tarehe 13 Septemba 2022. Kushoto ni mke wa Makamu wa Rais Mama Mbonimpaye Mpango na Askofu wa Jimbo la Kigoma Mhashamu Joseph Mlola, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Bugando Dkt. Fabian Massaga na Kulia ni Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel na Askofu wa Jimbo la Mwanza Mhashamu Renatus Nkwande.
……………………….
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amewaasa wananchi wa mkoa wa Mwanza na kanda ya ziwa kwa ujumla wanaojishughulisha na uvuvi kuacha kutumia dawa zisizofaa katika uhifadhi wa Samaki ili kuepukana na ongezeko la wagonjwa wa saratani katika mkoa mkoa huo.
Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 13 septemba 2022 wakati akizindua Jengo la Wodi ya Wagonjwa wa Saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando iliopo Jijini Mwanza. Amezitaka mamlaka za udhibiti kuhakikisha wanakomesha jambo hilo mara moja.
Makamu wa Rais amesema serikali inawekeza katika ujenzi wa miundombinu ili kuhakikisha huduma za matibabu ya saratani zinasogezwa karibu na wananchi. Ameongeza kwamba takwimu zinaonesha kuwa ugonjwa wa saratani bado ni miongoni mwa magonjwa yanayoongoza duniani kwa kusababisha vifo kwa watu wengi ambapo nchini Tanzania takribani watu 42,000 kila mwaka hupata ugonjwa huo wa saratani.
Makamu wa Rais amelishukuru Kanisa Katoliki na Madhehebu mengine kwa kuendelea kushirikiana na Serikali kusogeza huduma za jamii ikiwemo afya karibu na wananchi. Amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na wadau wengine ili kuendelea kuboresha huduma za afya hapa nchini.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema Tanzania imekuwa nchi ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuanzisha kiwanda cha mionzi dawa kitakachosaidia utoaji huduma kwa wagonjwa wa saratani.
Aidha Dkt. Mollel amewaasa viongozi wa dini kuhamasisha waumini wao kuwa na bima za afya kwa usalama wa afya zao pamoja na kuwa na uhakika wa mapato ya kuendesha vituo vya kutolea huduma za afya.
Awali akitoa taarifa za Ujenzi wa Wodi hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando Dkt. Fabian Massaga amesema kukamilika kwa Jengo hilo kumeleta unafuu mkubwa kwa wananchi wa kanda ya ziwa ambao wanapata huduma za matibabu, kupungua kwa gharama za wagonjwa waliokuwa wakipata malazi kutoka nje ya hospitali pamoja na wagonjwa kufuatilia huduma za tiba kwa usahihi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi wa Hospitali ya Bugando Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mwanza Mhashamu Renatus Nkwande, ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuendeleza ushirikiano na kanisa hilo katika kuhudumia wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya.
Amesema ujenzi wa Jengo hilo utaokoa Maisha ya watu wengi wanaokubwa na madhila ya saratani ndani na nje ya Tanzania. Askofu Nkwande ameiomba serikali kuisaidia hospitali hiyo kupata mashine, vifaa pamoja na samani zitakazorahisisha katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa saratani.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza na wananchi mbalimbali waliofika kupata tiba katika Jengo la Wodi ya Wagonjwa wa Saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando Jijini Mwanza mara baada ya uzinduzi wa Jengo hilo leo tarehe 13 Septemba 2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia wananchi, wauguzi pamoja na viongozi wa dini na serikali mara baada ya kuzindua Jengo la Wodi ya Wagonjwa wa Saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando Jijini Mwanza leo tarehe 13 Septemba 2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiagana na Askofu wa Jimbo la Kigoma Mhashamu Joseph Mlola wakati alipomaliza shughuli ya Uzinduzi Jengo la Wodi ya Wagonjwa wa Saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando Jijini Mwanza leo tarehe 13 Septemba 2022. Kulia ni Askofu wa Jimbo la Mwanza Mhashamu Renatus Nkwande.