Featured Kitaifa

WANANCHI WAASWA KUTOA TAARIFA ZA KUFICHUA UKATILI WA KIJINSIA UNAOENDELEA KATIKA JAMII

Written by mzalendoeditor

Na Eva Godwin – Dodoma

TAASISI ya Kituo Cha Msaada Wa Sheria Kwa Wanawake (WLAC) imeiasa  Jamii kuwa na ushirikiano wa kutoa  taarifa za kufichua ukatili wa kijinsia unaoendelea katika maeneo mbalimbali 

Wakili wa kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC) Abia Richard akizungumza na Mzalendo blog leo Septemba 12, 2022 kwenye wiki ya maonesho ya maadhimisho ya Miaka 20 ya Tume ya Haki za Binadamu na Utaswala bora yanayofanyika katika viwanja vya Jakaya Kikwete ambapo Taasisi mbalimbali za Msaada wa sheria zimeshiriki Jijini Dodoma.

Amesema Jamii inapaswa kuwa mstari wa mbele katika kupaza sauti kwa kufichua ukatili hasa kwa wale Watu wanaoficha ukatili unaoendelea katika Jamii zetu.

“Jamii inatakiwa kuwa msaada kabisa katika kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia kwa wanawake na Jamii isipochukua hatua sisi tutashindwa kutatua hizi shida
Kama Jamii yenyewe ikifumbia macho huu ukatili unaoendelea kwenye Jamii zetu hivi vitendo havitaweza kukoma wala kuisha, tusiofie kupoteza ndugu au wenzi wetu kwa kuficha hivi vitendo vya kikatili”, amesema

” Jamii hionyeshe ushirikiano kwa kupaza sauti zao kwenye vyombo husika, kuna mwingine anashindwa kutoa taarifa kwa kuhofia labda akijulikana itamletea shida, lakini pale ambapo unakaa kimya ndipo unaendelea kulikuza tatizo na mwisho wa siku ndio madhara makubwa yanatokea”. Amesema Wakili Richard

Aidha Amesema wao kama taasisi zisizo za kiserikali pia wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali katika kujitahidi kufikisha msaada kwenye jamii .

“Moja ya changamoto ni utekelezaji katika kesi unaweza ukakuta Wakili amefanya kesi imeisha kwa wakati na hukumu imeenda kwa wakati lakini mteja kupata kile ambacho kimeamriwa kwenye hukumu inakuwa inachukua muda mrefu sana ambapo unakuta sasa mteja anasubiri kwa muda huo mrefu kusubiri haki yake, na haki iliyocheleweshwa ni sawasawa na haki iliyonyimwa”, amesema

“Katika kuendelea kuelimisha jamii juu ya sheria na haki za binadamu ni fedha kwasababu sisi ni taasisi binafsi hivyo tunategemea wadhamini watusaidie tuweze kuendelea na majukumu, kwasababu kilakitu kinategemea fedha kun kuandaa semina na mafunzo mbalimbali kuhusu sheria na haki za binadamu, kutoa machapisho mbalimbali, kufanya utafiti na kutumia matokeo ya tafiti hizo kama zana na ushawishi hivi vyote vinategemea fedha na huduma zinakuwa zinalegalega kwa kuwa na changamoto hiyo”. Amesema Richard

Ameongezea kwa kutoa wito kwa vyombo vya sheria viweze kuhakikisha vinatoa haki kwa mapema kwa utekelezaji wa haraka na haki iwe sawa kwa sawa kwa pande zote mbili.

” Nipende tu kutoa wito kwa vyombo vyetu vya sheria kuhakikisha wanatoa haki kwa muda unaostahili kama hukumu imeshasema basi utekelezaji ufanyike kwa haraka na haki iwe sawa kwa kila Mmoja”. Amesema

About the author

mzalendoeditor