Baadhi ya wanafunzi wa Sekondari ya bweni ya wasichana ya Nyankumbu wakiwasikiliza viongozi na wafanyakazi wanawake wa Kampuni ya GGML ambao waliwapatia mafunzo ya siku mbili kuhusiana na malezi ya kitaaluma kwa wanafunzi hao wa kike mkoani Geita.
…………………………………………..
NA MWANDISHI WETU
Katika jitihada za kuhakikisha jamii inanufaika kutokana na shughuli za uchimbaji dhahabu nchini, wafanyakazi wanawake wa Kampuni ya Geita Gold Mine Limited (GGML) wameendesha semina ya siku mbili kwa ajili ya kutoa malezi ya kitaaluma kwa wanafunzi wa kike mkoani Geita.
Semina hiyo iliyofanyika juzi Mjini Geita katika Shule ya Sekondari ya bweni ya wasichana ya Nyankumbu iliyojengwa na GGML, imeasisiwa na kampuni hiyo kupitia Umoja wa Watumishi Wanawake wanaofanya kazi mgodini unaojulikana kwa jina la GGM ladies.
Akizungumza kwa niaba ya menejimenti ya GGML, Meneja Mwandamizi – Mawasiliano na Mahusiano, Manace Ndoroma amesema wanawake wanaofanya kazi mgodini, wamekuwa mstari wa mbele kuhamasisha umuhimu wa nafasi ya mwanamke katika jamii hususani.
Pia wametoa hamasa kwa mwanamke anayefanya shughuli zinazotokana na uchimbaji madini au biashara inayotokana na mnyororo wa thamani katika sekta ya uchimbaji.
Amesema GGML kupitia umoja huo imekuwa ikitoa misaada ya hali na mali ikiwemo fedha na vifaa mbalimbali kwa makundi maalumu ndani ya jamii yetu ili kuhakikisha jamii inayozungukwa na shughuli za uchimbaji wa dhahabu inafaidika kutokana na uwepo kampuni hiyo.
“Tumekuwa mstari wa mbele kushirikiana na Serikali kuhamasisha masuala ya usawa wa kijinsia. Mtakumbuka tarehe 26 Agosti mwaka huu ilikuwa siku ya usawa wa wanawake duniani. GGML tulitoa elimu kubwa kwenye mitandao yetu ya kijamii na vyombo vya habari juu ya nafasi muhimu ya mwanamke katika jamii.
“Tumekuwa tukifanya hivyo pia hata katika matukio ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kila tarehe 8 Machi,” alisema Ndoroma na kuongeza kuwa semina hiyo ni mwarobaini wa changamoto za wanafunzi wa kike kufahamu taaluma sahihi za kuchagua katika maisha baada ya kuhitimu elimu ya sekondari.
Amesema kumekuwepo changamoto ya wasichana wengi hususanI katika mwaka wao wa mwisho wa masomo au baada ya kumaliza elimu ya sekondari kushindwa kufahamu hatima ya masomo wanayoyasomea na uhalisia wa watakachokutana nacho katika elimu ya juu au baadae kwenye soko la ajira.
“Sisi menejimenti ya GGML tuliona ni vyema tuandae semina hii ili hata watakaopenda kuchagua nyanja mbalimbali za taaluma na hata kuwa wachimbaji au viongozi waandamizi katika kampuni za uchimbaji dhahabu ikiwemo GGML, wafikie ndoto zao kwa kuwaona akina mama wanaofanya vizuri katika taaluma hiyo tuliokuja nao kutoka GGML,” alisema Ndoroma.
Akihutubia kwa niaba ya serikali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Prof. Godius Kahyarara amewataka wadau mbalimbali nchini kuchangia maendeleo ya elimu nchini hususani kwa mtoto wa kike badala ya kuiachia serikali jukumu hilo pekee yake.
“Nawapongeza sana GGM kwa kuonyesha mfano mzuri wa wadau wanaochangia maendeleo ya elimu. Bahati nzuri nchi yetu imeendelea kuwa na mfumo mzuri wa elimu bora ukilinganisha na nchi zingine. GGM wanao mchango mkubwa katika uchumi wa nchi yetu kutokana na kodi wanayolipa.
“Jitihada kubwa wanayoionyesha katika jamii imeleta matokeo chanya ikiwemo kujenga miundombinu ya elimu na mafunzo kama haya yanayoleta tija kubwa katika jamii. Bahati nzuri mafunzo haya yanatolewa kwa wasichana wenye umri mdogo jambo ambalo sio rahisi kulisahau,” alisema Prof Kahyarara.
Akihamasisha wanafunzi kufikia ndoto zao katika Shule ya Wasichana Nyankumbu, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita, Zahara Michuzi ameipongeza GGML na wafanyakazi wanawake wanaofanya kazi katika kampuni hiyo kwa kuandaa mafunzo hayo yanayotoa mwangaza kwa wanafunzi wengi wa kike kujitambua na kufikia malengo sawa na viongozi wa kike waliofanikiwa katika nafasi mbalimbali.
“Binafsi hata mimi sijafika hapa kwa nguvu zangu mwenyewe. Nilijitambua, nikamtanguliza Mungu lakini pia nikaomba watu mbalimbali akiwemo Profesa Peter Msofe wakati anafundisha Chuo Kikuu cha Dodoma kunipatia malezi ya kitaaluma ambayo yamenisaidia hadi kufikia hatua hii ya kuongoza Halmashauri ya Mji Geita kwa mafanikio,” alisema Zahara Michuzi.
GGML imekuwa kinara wa uwekezaji kwenye jamii tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000 ambapo vipaumbele vikuu vimekuwa ni miradi ya afya, elimu, maji, barabara, miradi ya kukuza kipato na miradi mingine mingi ya kijamii ili kuhakikisha jamii mwenyeji inapata maisha bora.
Kampuni imejenga zaidi ya shule saba za Msingi na tano za Sekondari ndani ya Mkoa wa Geita kwa kipindi cha miaka minne iliyopita.
Mapema mwaka huu, GGML iliibuka mshindi wa jumla katika kampuni zinazofanya vizuri kwenye sekta ya madini nchini Tanzania kwa mwaka 2020/2021 baada ya kunyakua tuzo katika vipengele vya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii, mazingira, usalama, mlipaji bora wa kodi na uendelezaji wazawa.
Baadhi ya wanafunzi wa Sekondari ya bweni ya wasichana ya Nyankumbu wakiwasikiliza viongozi na wafanyakazi wanawake wa Kampuni ya GGML ambao waliwapatia mafunzo ya siku mbili kuhusiana na malezi ya kitaaluma kwa wanafunzi hao wa kike mkoani Geita.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita, Zahara Michuzi (kushoto) akizungumza katika mafunzo ya siku mbili yaliyoandaliwa na wafanyakazi wanawake wa Kampuni ya GGML kwa lengo la kuwapatia malezi ya kitaaluma wanafunzi wa kike mkoani Geita. Katikati ni Mkuu wa Shule ya Sekondari ya bweni ya wasichana ya Nyankumbu, Georgia Mugashe na kulia ni Meneja Mwandamizi – Mawasiliano na Mahusiano kutoka GGML, Manace Ndoroma.
Meneja Mwandamizi – Mawasiliano na Mahusiano kutoka GGML, Manace Ndoroma akizungumza katika semina hiyo.