Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Butiama,Jumanne Sagini akishiriki kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Mkoa wa Mara uliofanyika katika Viwanja vya Mkendo vilivyopo Musoma mjini, mkoani Mara
………………………………..
Na Mwandishi wetu,
Mbunge wa Jimbo la Butiama na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini (MB) ametoa pongezi kwa viongozi wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo TCCIA Mkoani Mara kwa kuandaa maonesho ya Biashara yaliyowakutanisha wafanyabiashara mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mbunge Sagini alisema licha ya kuwa ni mara ya kwanza kwa maonesho hayo ya biashara kufanyika mkoani Mara, TCCIA wamefanikiwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wa biashara kutoka ndani na nje ya nchi.
“Niombe kwa kuwa tumesema ni mara ya kwanza isiwe ndio mara ya kwanza na mwisho bali iwe endelevu. Mwanzo huwa ni mgumu ila kwa Mara wamefanikiwa sana”
Mbunge Sagini alisema hayo baada ya kutembelea baadhi ya mabanda yaliyopo katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara mkoa wa Mara yaliyofanyika katika uwanja wa Mkendo, Musoma Mjini.
Aidha Mbunge Sagini amewataka Watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii walioshiriki kwenye Maonesho hayo kuwa mfano wa kupanda miti na kuwafundisha wananchi namna ya kilimo bora cha misitu hususani katika milima ya Kyanyari na Buturu inayopatikana Wilayani Butiama ili kuendelea kutunza mazingira ya nchi yetu.
Pia Mbunge wa Jimbo la Butiama na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini amewataka vijana wa Mkoa wa Mara kutumia fursa zilizopo Mkoa wa Mara kutengeneza ajira ili kuondokana na vitendo vya uhalifu.
“Niwasihi vijana kutumia fursa zilizopo Mkoani Mara kutengeneza ajira na kuwafanya wawe bize ili kujiepusha na vitendo vya uhalifu”
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Butiama,Jumanne Sagini akishiriki kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Mkoa wa Mara uliofanyika katika Viwanja vya Mkendo vilivyopo Musoma mjini, mkoani Mara
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Butiama,Jumanne Sagini akizungumza na Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mara,Boniphace Ndengo na kuipongeza Taasisi yao kwa kuandaa maonyesho ya Biashara mkoani Mara yaliyowakutanisha wafanyabiashara mbalimbali nchini.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Butiama, Jumanne Sagini akiteta jambo na Balozi wa Zimbabwe,Meja Jeneral Anselem Nhamo Sanyatwe aliyefika kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Mkoa wa Mara uliofanyika uwanja wa Mkendo kilichopo Musoma mjini,mkoani Mara.