Featured Kitaifa

WAZIRI MKENDA AITAKA TIMU YA KUCHUNGUZA UTOAJI MIKOPO ELIMU YA JUU KUMALIZA KAZI NDANI

Written by mzalendoeditor

Na Mathias Canal, WEST-Dar es salaam

Timu ya watu watano imeanza kazi rasmi leo tarehe 5 Septemba 2022 ya kufuatilia utoaji mikopo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2017/2018 hadi mwaka 2021/2022.

Timu hiyo itakayofanya kazi ndani ya mwezi mmoja itaongozwa na Prof Allan Mushi ambaye ni mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro, na wajumbe wake ambao ni Idd Makame kutoka Zanzibar na Dkt Martin Chegere ambao wote kwa pamoja ni wataalamu wa mifumo waliobobea katika sayansi ya Kompyuta na Takwimu.

Akitangaza kuanza kazi kwa timu hiyo Jijini Dar es salaam katika ukumbi wa mikutano wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu-HESLB wakati wa kikao kazi cha Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya HESLB, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda amesema kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa malalamiko yanayotolewa kuhusu Bodi ya Mikopo yanapatiwa ufumbuzi.

Waziri Mkenda amesema kuwa serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan imeongeza Bajeti hadi kufikia Bilioni 570 za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu hivyo ni lazima kuwe na usimamizi wa uangalizi wa hali ya juu.

“Hatufanyi hivi kwa sababu ya kuumbuana ila ni kwa sababu ya kutaka uwazi na uwajibikaji na kwa sababu hiyo ni lazima kutoa mikopo kwa haki na vigezo stahiki vilivyowekwa na serikali bila kujuana” Amekaririwa Waziri Mkenda

“Shunguli za elimu zinahitajika kwa kila mtu hivyo ni wajibu wetu kufanya kwa haki na uwajibikaji uliotukuka, hatutatoa mikopo kwa kujuana kwa undugu, urafiki, au ujamaa hakuna (Lobbying), tunataka haki”

“Na kwenye hili tunakaribisha watu watoe taarifa kwa sababu kama kuna mtoto wa Mkenda uliyesoma nae utakuwa unamjua baba yake ni nani na uwezo wake, halafu wewe unaona mtu huyo amepewa mkopo toa taarifa” Amesisitiza Waziri Mkenda na kuongeza kuwa

Prof Mkenda amesema kuwa Mtu yeyote ambaye ana wasiwasi na utoaji wa mikopo anakaribishwa ili aweze kuisaidia timu kufanya kazi yake kwa kuwa na taarifa zenye usahihi wa hali ya juu kutoka kwa wanachi husika.

About the author

mzalendoeditor