Featured Kitaifa

MRADI WA TIMIZA MALENGO SULUHISHO KWA VIJANA WA RIKA BALEHE

Written by mzalendoeditor

Makamu Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI Mhe. Dkt Alice Kaijage ,akizungumza na wanufaidika wa Mradi wa Timiza malengo (hawaonekeni katika picha) mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo unaoratibiwa na TACAIDS kwa ufadhili wa global fund wakati wa ziara ya kamati hiyo tarehe 3Septemba,2022 Mkoani Morogoro aliyekaa kulia kwake ni Mhe. Hanji Godigodi Mkuu Wilaya ya Kilombero, akifuatiwa na Bw. Kassim Nakapala Mwenyekiti wa Halimashauri ya Ifakara na kushoto kwake ni Bw. Kaspar Mmuya Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu akifuatiwa na Dkt.Leonard Maboko Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS.

…………………………………..

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI imeipongeza Serikali kwa ubunifu wa Miradi inayosadia vijana kuwajengea uwezo wa kujiamini na kuimarisha uchumi wao ili kujikimu kimaisha wakiwa salama dhidi ya maambukizi ya VVU na UKIMWI .

Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Kadumu ya Bunge na Masuala ya UKIMWI,Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe Dkt Alice Kaijage alisema hatua ya serikali kuanzisha Miradi hii ikiwemo Mradi wa Timiza Malengo wenye lengo la kuwasaidia wasichana rika balehe na wanawake vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 24 na waliopo nje ya shule kuwezeshwa kijamii na kiuchumi ili kujikimu kimaisha wakiwa salama dhidi ya VVU na UKIMWI ni jambo la kupongeza serikali kwakuwa miradi hii inahudumia vijana ambao ndio tegemeo la kesho.

“Kila mmoja anatambua uwepo wa maambukizi ya VVU lakini hatua hii inayochuliwa na serikali kupitia TACAIDS ya kukinga vijana wa Taifa hili ni jambo la kupongezwa sana,sisi kama wabunge wito wetu ni kuendelea kuishauri serikali kuongeza bajeti ili vijana wengi wa nchi hii weweze kunufaika” alisema Mhe Kaijage.

Mhe Kaijage aliongeza kuwa matokeo ya Mradi wa Timiza malengo yanaoenekana kwa macho kwani vijana walionufaika kupitia mradi huo tumewaona na miradi yao inaendelea kukuwa kupitia mtaji mdogo wanaopatiwa kupitia mradi wa Timiza Malengo. vijana hao ni wale waliotoka katika mazingira magumu ambao kwa sasa tayari wamekuwa walimu wazuri kwa wenzao. 

Baadhi ya vijana waliotembelewa na kamati ya bunge ambao tayari wanaendesha miradi tayari wameweza kuwahamasisha vijana wenzao na kujiunga katika vikundi kwa lengo la kujipatia mikopo ya serikali ili kuendelea kujikwamua kiuchumi.

Baadhi ya vijana wanaonufaika na Mradi huo walieleza jinsi wanavyofaidika na mradi katika kujikomboa kiuchumi, vijana hao hupatiwa shilingi 250,000 za Kitanzania ambazo zimewasaidia kuanzisha miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ufugaji,kilimo, biashara,  kulea na kusomesha watoto wao bila kuwa tegemezi, pia wameweza kuunda vikundi vya wasichana wenzao ambavyo vinaweza kuwapa sifa za kupata mkopo wa Halimashauri.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilomberao Mhe Hanji Godigodi alisema mradi huu unamanufaa makubwa katika Mkoa wa Morogoro kutokana na mafanikio yanayoendelea kuonekana kwa vijana wote waliopo kwenye mradi, wale ambao bado wapo shuleni lakini pia walio nje ya shule.

“Mradi huu umesaidia sana vijana lakini naomba kupitia mradi huu wa Timiza Malengo zinunuliwe runinga na kuandaliwa CD ambazo zinamafunzo ambayo wanafunzi wakiandaliwa utaratibu wa kuangalia runinga hizo kwa utaratibu wa shule husika na kupatiwa mitihani inayoendana na mada husika itawasidia kuwajengea ufahamu zaidi na kufuatilia namna sahihi ya kujikinga na maambukizi ya VVU pamoja na magonjwa mengine yatokanayo na ngono” alisema Godigodi.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu Bw. Kaspar Mmuya ametoa shukrani kwa wakazi wa Ifakara ambao wameupokea mradi huu na kutekeleza kwa vitendo malengo ya Mradi huu ambao unapambana na changamoto zinazowakumba wananchi za hali duni ya kimaisha ambapo mradi huu umeweza kutatua tatizo la kiuchumi la kusaidia kuanzisha miradi midogo midogo. 

Bw. Kaspar ameongeza kuwa mwaka huu serikali imeanzisha mpango rasmi wa kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi ya VVU kwa wanafunzi wote walio katika shule za serikali na binafsi, katika halimashauri 18 nchini. kwakuwa watoto walio katika rika balehe ndio waliokatika mazingira hatarishi ya kupata maambukizi ya VVU.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Leonard Maboko amefafanua kuwa wakati wanaanzisha mradi huu wa Timiza Malengo ni wakati ule kila mwaka kiwango cha maambukizi Mapya ya VVU yalipokuwa yakitokea asilimia 40 ya maambukizi mapya yalikuwa yanatokea kwa vijana walio katika umri wa miaka 15 hadi 24 na kundi hilo la vijana asilimia 80 ilikuwa ni vijana wa kike ambao ndio wasichana balehe na wanawake vijana.

Kutokana na hali hiyo ndio ilipelekea kuanzishwa kwa program hii ambayo ina masuala ya kibaolojia,mabadiliko ya tabia na masuala ya kimfumo (combination privention) lengo ni kukinga vijana wa kike wasipate maambukizi mapya ya VVU.

“Mprogramu hizi zilitekelezwa kuanzia shule za msingi kwa vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 24 ili waendelee kukaa shuleni na kutimiza malengo yao, na tafiti zinaonesha kuwa mtoto wa akikaa shuleni muda mrefu unamuepusha na vishawishi” alisema Dkt Maboko.

Vijana waliopo nje ya shule wanawezeshwa  kiuchumi kwa kuwa kuna wengine wanakuwa tayari wamepata watoto wakiwa katika umri mdogo kuwapata mabinti ambao bado wapo katika umri mdogo na wanatoka katika kaya masikini ambayo haitoshelezi kujikimu kimaisha, hivyo hao wanafundishwa elimu ya ujasiliamali pamoja na fedha kidogo kwa ajili ya biashara ambazo kwa kadri tulivyotembelea tumona miradi walioanzisha kutokana na fedha hizo zimekuwa ni mkombozi kwa vijana hao,ambao kwa sasa wameweza kujitegemea na kusaidia wategemezi wao.

Mradi wa Timiza Malengo unatekelezwa kwa ushirikiano baina ya Serikali,Amref na TAYOA ukiratibiwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania TACAIDS kwa ufadhili wa mfuko wa Dunia (Global Fund)wa kupambana na VVU na UKIMWI ,Kifua Kikuu na Malaria .

Mradi huu unatekelezwa katika awamu mbili ambapo ilianza Mikoa ya Dodoma,Singida,Morogoro, katika halimashauri tano na awamu ya pili mradi umetekelezwa katika halimashauri 18 kwa mikoa ya Dodoma,Morogoro,Singida ,Geita na Tanga. 

Makamu Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI Mhe. Dkt Alice Kaijage ,akizungumza na wanufaidika wa Mradi wa Timiza malengo (hawaonekeni katika picha) mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo unaoratibiwa na TACAIDS kwa ufadhili wa global fund wakati wa ziara ya kamati hiyo tarehe 3Septemba,2022 Mkoani Morogoro aliyekaa kulia kwake ni Mhe. Hanji Godigodi Mkuu Wilaya ya Kilombero, akifuatiwa na Bw. Kassim Nakapala Mwenyekiti wa Halimashauri ya Ifakara na kushoto kwake ni Bw. Kaspar Mmuya Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu akifuatiwa na Dkt.Leonard Maboko Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Bw. Jacob Kayange akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi wa Timiza Malengo wenye lengo la kusaidia wasichana rika balehe na wanawake vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 24 kwa kamati ya kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI ilipofanya ziara katika Mkoa wa Morogoro kwa lengo la kukakuwa utekelezaji wa mradi huo.

Mhe Hanji Godigodi akitoa salamu za Mkoa wa Morogoro kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI walipokuwa katika Ziara ya kutembelea mradi wa Timiza Malengo Sptemba 3, 2022.aliyekaa kushoto kwake ni Bw. Kaspar Mmuya Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halimashauri ya Kilombero akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi wa Timiza Malengo katika halimashauri yake wakati wa ziara ya kamati ya kudumu ya Bunge na Masuala ya UKIMWI aliyekaa kulia kwake ni Bw. Richard Ngirwa Mkurugenzi Sera na Mipango wa TACAIDS.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Kaspar Mmuya akifafanua dhima ya mradi wa Timiza Malengo ambao unaratibiwa na TACAIDS kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu,aliyekaa kushoto kwake ni Mhe Dkt Alice Kaijage Makamu mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI, na mwisho ni Dkt Leonard Maboko Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS.

Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt Leonard Maboko, akisalimia hadhara ya wanufaika wa mradi wa Timiza Malengo wakati wa ziara ya kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI walipotembelea Mkoa wa Morogoro kukagua ufanishi wa mradi huo wenye lengo la kuwasaidia wasichana rika balehe na wanawake vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 24 waliko shuleni na nje ya shule. aliyekaa kulia kwake ni Mhe Dkt Alice Kaijage,Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na aliyekaa mwisho kushoto ni Bw.Kaspar Mmuya Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na Uratibu

 Mjumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya masuala UKIMWI Mhe. Grace Tendega,akichangia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mradi wa Timiza malengo baada ya kuwasilishwa na watekelezaji wa mradi huo, ambapo alisisitizia umuhimu wa upatikanaji wa Kondomu za Kike.

Mjumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI Mhe Hawa Chakoma,akiipongeza TACAIDS kwa uratibu mzuri katika utekeelezaji wa Mradi wa Timiza Malengo na usambazaji wa Vishikwambi ambavyo vinasaidia walimu kufundisha vijana namna ya kujikinga na Maambukizi ya VVU.

Mjumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI Mhe Antipas Mgungisi,akichangia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za UKIMWI iliyotolewa na wataalam alisisitizia umuhimu wa kufuatilia matumizi sahihi ya Kondomu zinazosambazwa serikali kupitia kwenye Makasha ya Kondomu kwenye maeneo hatarishi.

About the author

mzalendoeditor