Featured Kitaifa

WANANCHI BADO WANA MWAMKO MDOGO KUPATA CHANJO YA UVIKO-19 VISIWANI ZANZIBAR

Written by mzalendoeditor

MENEJA Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma kutokana Wizara ya Afya Zanzibar, Bakar Magarawa, amesema wananchi bado wana mwamko mdogo wa kupata chanjo ya UVIKO – 19.
Alisema hayo alipokuwa akiwasilisha mada kwa waandishi wa habari juu ya hali halisi ya maradhi hayo nchini na upatikanaji wa chanjo, katika mafunzo yaliyoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC) kwa kushirikiana na Internews.
Alisema lengo la serikali hadi kufika Disemba mwaka huu asilimia 70 ya wananchi wawe tayari wamechanjwa lakini hadi sasa waliochanjwa ni asilimia 35, hali inayoonesha kwamba kuna kundi kubwa halijahamasika kupata kinga hiyo.
Sambamba na hayo alifahamisha kwamba licha ya serikali na waandishi wa habari kufanya kazi kubwa ya kuihamasisha jamii juu ya umuhimu wa kuchanja bado jamii haijaona umuhimu huo.
Alisema kwa sasa vipo vituo zaidi ya 120 vinavyotoa chanjo hizo katika maeneo mbalimbali, hivyo aliiomba jamii ikavitumia ipasavyo ili kupata chanjo hiyo.
Alisema tokea walipoanza kutoa chanjo hiyo, watu 267,824 sawa na asilimia hiyo 35.10 wamechanjwa, hivyo aliwaomba waandishi wa Habari kuendelea kuhamasisha.
“Tunashukuru kazi kubwa inayofanywa na vyombo vya habari lakini bado tuendelee kwani wapo watu wengi hawajajitokeza hivyo ipo haja ya kuendeleza kupatiwa elimu,” alieleza Magarawa.
Akitaja miongoni mwa sababu zinazochangia jamii kutokubali kupata chanjo ni pamoja na dhana kwamba chanjo inapunguza nguvu za kiume, kukosa uzazi kwa wanawake na baadhi ya watu kuamini kwamba chanjo hizo zinasababisha watu kugeuka wanyama.
Aidha alifahamisha kwamba serikali zote mbili zimefanya uchunguzi na kubaini kwamba chanjo hizo ni salama, hivyo alitumia fursa hiyo kuihamasisha jamii kukubali kupata kinga.
“Serikali imeandaa miongozo mbali mbali ili kukabiliana na ugonjwa huo ikiwemo kupata chanjo na mambo mengine, hivyo ni vyema wananchi kwenda sambamba na mikakati ya serikali ili kuweza kuwa na afya bora,” aliongeza Meneja huyo.
Aidha magarawa aliitaka jamii kuelewa kwamba ugonjwa huo bado upo na kwamba wagonjwa wanaendelea kupokelewa ambapo hadi Agosti 25, 2022 kulikuwa na wagonjwa watano katika hospitali ya Mnazimmoja ambao baadhi yao ni watalii na wengine ni wasafiri waliongia nchini kutoka nje ya nchi.
Akiwasilisha mada ya uandishi wa habari za UVIKO 19 na chanjo dhidi ya ugonjwa huo, Mkuu wa Idara ya mafunzo Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma Zanzibar ya chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Imane Duwe, aliwataka waandishi kuchukua tahadhari pale wanapokuwa katika majukumu yao ili wajikinge na maradhi hayo.
Aidha aliwasisitiza waandishi kuzingatia maadili na kuhakikisha taarifa zinahusu wagonjwa na ugonjwa huo na kuzifanyie uchunguzi lakini pia kuziwasilisha kwa kutumia lugha nyepesi kuepusha upotoshaji kwa umma.
Kwa upande wa Mwanasheria na Mwandishi wa Habari wa Shirika la Magazeti ya Serikali, Juma Khamis Juma, alisema ugonjwa wa UVIKO – 19 uliathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa habari na uhuru wa kujieleza.
Juma alieleza hayo alipokuwa akiwasilisha mada katika mafunzo hayo na kueleza kuwa hali hiyo ilisababisha waandishi wa habari kufanya kazi katika mazingira magumu na wakati mwengine kunyimwa taarifa muhimu zinazohusiana na ugonjwa huo.
Alisema baadhi ya vikwazo vimeondoka na kutoa rai kwa waandishi wa habari kuendelea kuihamasisha jamii kupata chanjo kwa sababu kwa sasa upatikanaji wa chanjo hiyo umerahisishwa.
Akifunga mafunzo hayo, Mwenyekiti wa ZPC, Abdalla Abdulrahman Mfaume, aliwataka waandishi kuyatumia mafunzo hayo ili yalete tija katika kazi zao.

About the author

mzalendoeditor