Featured Kitaifa

MORUWASA YAWATOA HOFU WAKAZI WA KATA YA MINDU

Written by mzalendoeditor
Na Farida Mangube, Morogoro
MENEJIMENTI ya Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa mazingira Mkoa wa Morogoro, (MORUWASA) imewaondoa hofu wananchi wa Kata ya Mindu wanaotegemea tanki la kuhifadhi maji la Kasanga kuwa mradi huo ambao uko kwenye kipindi cha matazamio baada ya mkandarasi kukamilisha kuwa umejengwa kwa kiwango kinachotakiwa na wataondokana na kero ya maji.
Mkurugenzi Mtendaji wa MORUWASA mhandisi Tamimu Katakweba alisema hayo baada ya yeye na wataalamu wa Mamlaka hiyo kutembea kwa miguu umbali wa zaidi ya kilometa sita kutoka kituo cha kusafisha na kutibu maji cha Mafiga hadi milimani lilipojengwa tanki la Maji la kasanga.
Lengo la ukaguzi huo ilikuwa ni kukagua maeneo yalipopita mabomba ya maji ili kujiridhisha kama kuna mapungufu yanayotishia upatikanaji wa maji baada ya maelekezo ya Mbunge wa Morogoro mjini Abdul-Aziz Abood baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kuhusu uhaba WA maji unaochangiwa na maeneo mengi mabomba kuvuja.
Hata hivyo Mhandisi Katakweba akabainisha ukaguzi huo ulibaini maeneo manne yaliyokuwa yakivuja maji na kwamba hilo ni jambo la kawaida la kiufundi na wanapopewa mrejesho wa taarifa huwarahisisha kugundua na kufanyia kazi mapema.
Akasema licha ya mivujo hiyo ya kawaida ya kiufundi ambayo wanaendelea kuidhibiti bado haijaathiri maji kufika kwenye tanki hilo la Kasanga linalopokea Lita 135,000 za maji ndani ya masaa matatu na kurudi kusambazwa kwa wananchi.
“Kazi kubwa ya mkandarasi ilikuwa ni kuhakikisha maji yanapanda kwa kiwango kinachotakiwa, mwanzo yalilazwa mabomba ya inchi mbili, baadaye nne na sasa tumeweka mabomba makubwa ya chuma ya inchi sita, na yanapandisha maji kwa kiwango kinachotakiwa”Alisema Mkurugenzi huyo.
Akasema kazi iliyobaki sasa ambayo ni jukumu lao na sio la mkandarasi ni kuhakikisha maji yanasambazwa na kufika kwa wananchi.
“Niwahakikishie wananchi zaidi ya 10,000 wa Mgaza na Kasanga kuwa watapata maji ya kutosha, badala ya ule mgao wa maji wa mara moja baada ya siku kumi Hadi 14, sasa watakuwa wanapata maji hata kila baada ya siku moja”Alisema Mkurugenzi huyo wa MORUWASA.
Baadhi ya Viongozi wa CCM wa Kata hiyo akiwemo Katibu Mwenezi wa kata Christina Adamu, walifika lilipo tenki hilo na kushuhudia maji yakiingia, na kusisitiza Mamlaka hiyo kuwapa taarifa viongozi ya Kile kinachoendelea ili nao wawaelimishe wananchi na kupunguza malalamiko.
“Shida kubwa ya wananchi ni maji, yakipatikana hakuna ugomvi, mwanzo tulisikia hayafiki kwenye tanki, lakini nimejiridhisha yanafika, nzuri ni kuona ili isijitokeze tena kama 2016 ambapo walisema maji yanazinduliwa kumbe yalibebwa na maboza na hatukuendelea tena kupata maji”Alisema Mwenezi huyo.
Siku moja kabla ya Ukaguzi huo, Mbunge wa Morogoro mjini Abdulaziz Abood, alifika mtaa wa Mgaza Kasanga, Kata ya Mindu manispaa ya Morogoro na kupokea kero ya malalamiko ya maji, huku wananchi wakidai Maji yalikuwa hayafiki kwenye tanki kutokana na mivujo mingi kwenye bomba linalopeleka maji kwenye tank.
Abood akaagiza Mkurugenzi wa MORUWASA kufanya ukaguzi katika miundo mbinu hiyo ya maji ili kujiridhisha na malalamiko hayo ya wananchi kwasababu mradi huo bado ni mpya.
Awali katika mkutano na viongozi mbalimbali wa CCM na wa Serikali katika Kata hiyo, Mkurugenzi wa huduma za usambazaji maji BetramMinde, alisema mradi huo maji Kasanga uko kwenye matazamio baada ya kuwa umekamilika ambapo mabomba ya inchi sita yanasambazwa.
Aidha akasema eneo la mtaa wa Mindu Kata ya Mindu, usanifu umeshafanywa ambapo watajenga tanki la mita za ujazo 500.

About the author

mzalendoeditor