Featured Kitaifa

RC SENDIGA AKABIDHI PIKIPIKI 7 KWA WATENDAJI WA KATA MANISPAA YA SUMBAWANGA

Written by mzalendoeditor
Na.OMM Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga amekabidhi pikipiki saba (7 ) kwa watendaji wa kata mkoani humo zenye thamani ya Shilingi milion 24 kwa ajili ya kuwasaidia katika utendaji wao wa kazi ikiwa ni pamoja na kusimamia miradi ya maendeleo Katika kata zao na usimamizi na ukusanyaji wa mapato.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema hayo leo mjini Sumbawanga (22.08.2022) ambapo pia ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kwa kuimarisha maeneo ya ukusanyaji mapato kwa kuhakikisha watumishi wanakuwa na vitendea kazi kwani ubunifu wa kuwagawia watendaji pikipiki utaongeza tija.
Sendiga ametoa wito kwa watendaji wa kata kutoa taarifa mapema kuhusu  mashine za kukusanyia mapato ( POS) ambazo zina changamoto ili ziweze kutatuliwa ili halmashauri iwe na uhakika wa fedha za kutekeleza miradi.
Kuhusu miradi Sendiga amewataka wataalamu na watumishi wengine kuhakikisha Miradi inamalizika kwa muda uliopangwa kwenye mkataba ili kupisha uanzishwaji wa Miradi mingine.
Pia kuhusu fedha za mikopo ya vikundi wanaokopeshwa hizo Sendiga ameagiza  wapewe elimu ili waweze kuanzisha Miradi itakayowasaidia kuinua vipato vyao na kuwapa uwezo wa kurejesha Mikopo kwa wakati.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya amesema mkakati uliopo ni kuhakikisha watendaji wa kata na mitaa wanapatiwa vitendea kazi ili waweze kusimamia na kuhamasisha shughuli za Maendeleo.
Mtalitinya alionya watendaji waliopatiwa pikipiki hizo kuwa wazitumie kwa kazi za wananchi na si kwenye shughuli binafsi na kuwa mfumo wa ufuatiliaji matumizi yake umewekwa vizuri.

About the author

mzalendoeditor