Featured Kitaifa

SHAKA: CCM INAFUATILIA KWA KARIBU UTEKELEZAJI MKAKATI WA KUWAKWAMUA VIJANA

Written by mzalendoeditor

Asema Chama hakitatazama Itikadi katika kuwanufaisha vijana

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kinafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mikakati ya kuwakwamua vijana dhidi ya umasikini, huku kikiwataka watumishi wa umma kutafsiri kwa vitendo juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kuwatengenezea vijana fursa za kujikwamua kiuchumi.

Hayo yamesemwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, alipokuwa akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Ifuta, Kata ya Ukondamoyo wilayani Urambo alipokagua ujenzi wa kituo cha Afya Ifuta.

Rais ameonyesha njia, njia ya kwanza ni kushusha fedha nyingi katika Halmashauri zetu za Wilaya kwa ajili ya kujenga au kuanzishwa kwa miradi ya maendeleo. Tuliahidi ajira milioni nane katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa vijana na wanawake mpaka ifikapo mwaka 2025.

“Kazi kubwa anayoifanya Rais Samia ni kutumia fedha za ndani kutengeneza fursa za ajira ili wananchi wajikwamue kiuchumi. Ni jukumu la watendaji wa serikali kutafsi kwa vitendo ili lengo hilo litimie na wananchi hususan vijana na wanawake wakwamuliwe kiuchumi.

Shaka amesema CCM itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mkakati wa serikali ili ahadi ya Chama kupitia Ilani ya Uchaguzi itekelezwe na kufikia malengo.

Aidha, amesema katika kuwakwamua vijana CCM haitatazama Itikadi yoyote bali inataka kuona fursa zinapatikana na wote wananufaika.

About the author

mzalendoeditor