KATIBU wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said (kulia), akimkabidhi zadi meneja wa benki ya DTB, Juma Burhan, baada ya kuwasilisha mada ya ujumuishaji vijana kwenye shughuli za ujasiriamali.
……………………………….
NA MWANDISHI WETU
VIJANA nchini wametakiwa kutumia fursa zinazowazunguka ili kujikwamua na changamoto mbali mbali zinazowakabili.
Akifungua mdahalo Mdahalo wa Kijana Imara Transformative, ulioandaliwa na shirika la Kiona Youth Coordinates (KYCo), ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana inayoadhimishwa Agosti 12 ya kila mwaka, uliofanyika katika hoteli ya Golden Tulip Zanzibar, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Ahmed Said, amesema kufanya hivyo kutaongeza mchango wao katika taifa.
Ameeleza kuwa vijana wa Zanzibar na Tanzania kwa ujuumla wanakabiliwa na changamoto mbali mbali lakini wakitumia vyema mipango na mikakati ya kitaifa na kimataifa, watanufaika na kujikwambua katika lindi la umasikini.
Aidha alipongeza ushiriki wa AZAKI za vijana katika kubadilisha mitazamo na maisha ya vijana nchini jambo linalosaidia juhudi za serikali katika utatuzi wa changamoto zinazowakabili vijana.
Aliongeza kuwa vijana ni kundi kubwa katika jamii hivyo kuna umuhimu wa kuunganishwa kwa mawazo na nguvu zao ili kuepuka kupeleka nguvu zao katika mambo yasiyo na tija kwa taifa.
“Kwa kuzingatia kuwa vijana ni kundi kubwa hivyo kama hatutokua na njia nzuri ya kutumia ‘energy’ (nguvu) hizo, wataipeleka mahali ambapo sio sahihi na matokeo yake tunaweza kuharibikiwa kama taifa,” alieleza Mhandisi Zena.
Aidha alilipongeza shirika la KYCo kwa utekelezaji mzuri wa mradi wa ‘Kijana Imara’ unaolenga kuwawezesha vijana kubadilisha mitazamo yao kwani kufanya hivyo kutawanya waelekeze nguvu zao katika uzalishaji mali.
Akizungumza wakati wa mdahalo huo uliohudhuriwa na vijana zaidi ya 250 kutoka taasisi mbali mbali za vijana na Mabaraza ya vijana ya wilaya za Unguja, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fatma Hamad Rajab, alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuratibu na kusimamia mipango ya maendeleo ya vijana hivyo alipongeza mchango wa sekta binafsi kusaidia vijana.
Alisema vijana wana haki ya kutumia fursa zilizopo kujiimarisha kiuchumi na kupaza sauti zao ili kupiga hatua za kimaendeleo na kwamba wizara yake itaendelea kutoa kila aina ushirikiano kwa asasi za vijana na wadau wa maendeleo kufikia malengo ya vijana.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa KYCo, Fatma Fungo, alieleza kuwa mradi wa ‘Kijana Imara Transformative Dialogue’ ni ubunifu ulioasisiwa na shirika lake mwaka 2021 ili kutoa mchango wa vijana katika maendeleo ya taifa.
Aliongeza kuwa mradi umewafikia zaidi ya vijana million 3.8 huku lengo mahsusi likiwa ni kufanya uchechemuzi kupitia vyombo mbali mbali vya mawasiliano kuwafahamisha vijana na jamii juu ya sera ya vijana ya taifa ya maendeleo ya vijana (2007) Tanzania bara na sera ya vijana ya Tanzania Zanzibar.
Alifafanua kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuyaelewa maudhui yaliyomo katika sera hizo ili vijana washiriki katika utekelezaji wa wajibu wao kwa familia zao, jamii na taifa kwa ujumla.
Aidha fatma aliongeza kuwa midahalo hiyo inaakisi dhana ya ushirikiano kati ya serikali, wadau wa maendeleo na sekta binafsi na wanatarajia kujiwekea miongozo ya matumizi ya vituo rafiki vya upatikanaji wa taarifa na maarifa, uendeshaji wa mabaraza ya vijana, vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi na mitandao ya kijamii.
“Pia tunaangalia umuhimu wa kufanyia kazi ukomo wa malengo yaliyoainishwa katika ajenda 2063 ya Afrika tuitakayo (Africa We Want), Malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs) ajenda 2030, Dira ya Afrika Mashariki 2050 na Dira ya Maendeleo Tanzania 2025,” alieleza.
Katika mdahalo huo mada mbali mbali ziliwasilishwa na kujadiliwa na wataalamu wa masuala ya vijana, uchumi na afya ambapo vijana walioshiriki walipata fursa ya kujadili na kupatiwa ufafanuzi.
Siku ya kimataifa ya vijana huadhimishwa kila ifikapo Agosti 12 ya kila mwaka ambapo kwa Zanzibar kilelel cha wiki hiyo kitafanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Kikwajuni Zanzibar kikitarajiwa kuhudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
KATIBU wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said (kushoto), akimsikiliza Mkurugenzi wa Kiona Youth Coordinate, Fatma Fungo (kulia) baada ya kufungua mdahalo wa Kijana Imara Transformation uliofanyika hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar. Katikati ni Meneja wa DTB, Juma Burhan.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Fatma Hamad Rajab (kulia), akibadilishana mawazo na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Sharif Ali Sharif, walipokutana kwenye mdahalo wa Kijana Imara Transformation uliofanyika hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar.
KATIBU wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said (katikati walioketi), Mkurugenzi wa Kiona Youth Coordinate, Fatma Fungo (kulia) na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Fatma Hamad Rajab (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watendaji wa shirika la Kiona Youth Coordinate.
KATIBU wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said (kulia), akimkabidhi zadi meneja wa benki ya DTB, Juma Burhan, baada ya kuwasilisha mada ya ujumuishaji vijana kwenye shughuli za ujasiriamali.