Featured Kitaifa

DK.MSONDE ATAKA MAAFISA ELIMU NCHINI KUSIMAMIA MIRADI YA ELIMU

Written by mzalendoeditor

Asila Twaha, Tabora

Naibu Katibu Mkuu(Elimu) Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Charles Msonde amewataka Maafisa Elimu Mkoa na Maafisa Elimu Sekondari wa Halmashauri kusimamia miradi ya elimu kukamilika kwa wakati ili kuepuka hoja za ukaguzi katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Ameeleza hayo Agosti 15, 2022 Mkoani Tabora wakati akifungua kikao kazi cha Mafunzo ya Kuwajengea Uwezo Maafisa hao kuhusu Usalama wa Mazingira na Jamii katika kutekeleza mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (Tanzania Secondary Education Quality Improvement Project – SEQUIP) katika maeneo yao ili kuepuka changamoto zinazoweza kutokea katika utekelezaji wake.

Ameendelea kufafanua Serikali inaendelea kujenga na boresha miundombinu ya elimu na fedha za mradi wa SEQUIP ni kuboresha elimu ya sekondari, kuongeza fursa ya upatikanaji wa elimu, kupunguza vikwazo vinavyosababisha wanafunzi kuacha shule, kuwasaidia wanafunzi kumaliza elimu bora ya sekondari na kupunguza changamoto za upatikanaji wa elimu nchini.

Dkt. Msonde amewataka maafisa hao katika kusimamia ujenzi wa shule hizo kuepuka migogoro ya ardhi inayoweza kutokea na kusababisha matatizo kwa kutokuendelea kwa ujenzi, vilevile kusimamia ujenzi ili uendane na thamani ya fedha iliyotolewa, pia kusimamia utekelezaji wa ujenzi uzingatie muda uliowekwa ili ukamilike kwa wakati na shule hizo ziweze kutumika na wanafunzi kwa haraka.

“Ninyi ni wabobezi katika usimamizi na utekelezaji wa elimu tushirikiane sote ili miradi hii iwe yenye kuleta tija katika Taifa letu” amesema Dkt. Msonde

Awali akitoa maelezo mafupi Mkurugenzi Msaidizi Idara Usimamizi wa Elimu Ofisi ya Rais – TAMISEMI Bi. Hadija Mcheka ameueleza Naibu Katibu Mkuu Dkt. Charles Msonde kuwa, kikao hicho kitakuwa cha siku mbili kwa kujengewa uwezo kwa maafisa hao kwa kufundishwa mada mbalimbali kutoka kwa wataalam ili kujipa na kuzifahamu taratibu za usimamizi wa mradi na kupata nafasi ya kutoa maoni katika kufanikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi.

Naye Afisa Elimu Mkoa wa Tabora Bw. Juma Kaponda akiongea kwa niaba ya watendaji hao ameishukuru Serikali kwa kuendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya elimu na kuahidi kuisimamia kwa kutekeleza na kufuata sheria, miongozo na taratibu zinazowataka kwa kuhakikisha sekta elimu inakuwa na manufaa kwa Taifa.

About the author

mzalendoeditor